In Summary

• Migawanyiko imeibuka katika jamii ya  Kiislamu nchini Kenya baada ya kundi mmoja kupuuzilia mbali msimamo wa baadhi ya viongozi wa Supkem

Hassan Ole Naado

Migawanyiko imeibuka katika jamii ya  Kiislamu nchini Kenya baada ya kundi mmoja kupuuzilia mbali msimamo wa baadhi ya viongozi wa Supkem na kuunga mkono mchakato wa BBI.

Siku chahe tu baada ya wahubiri wa kiislamu wakiongozwa na Hassan Ole Naado wa Supkem kutangaza  kupinga mchakato wa BBI, kundi jingine la Supkem limejitokeza kukinzana na msimamo huo.

“Gari moshi limesonga, hatutaki kuachwa kituoni. BBI ni halisi. Kwa hivyo tunafaa kusonga mbele na kama kuna maswali, vile (Raila alisema), wakati wa mashauriano umeisha,” Yusuf Nzibo alisema.

Nzibo alisema kwamba yeye ndiye mwenyekiti halisi wa Supkem na kushtumu kundi la Naado kwa kujaribu kufanya mapinduzi. Alisema kwamba kesi iliyowasilishwa kuhusu mzozo wa uongozi wa Supken bado haijaamuliwa.

Barua ya naibu msajili mkuu wa mashirika Karen Ndegwa, Machi 12, 2020, ilimtambua Nzibo kama mwenyekiti.

Nzibo alizungumza siku moja tu baada ya baraza la kitaifa la waislamu pia kutangaza kwamba litaunga mkono ripoti ya BBI. Mwenyekiti Sheikh Juma Ngao alisema kwamba baraza hilo linaunga mkono marekebisho ya katiba.

Naado siku ya Jumapili aliongoza kundi moja la wahubiri wa kiislamu mjini Nairobi kukosoa ripoti na mapendekezo ya BBI. Alisema kwamba ripoti hiyo inabuni rais mwenye mamlaka makubwa sana.

Naado na kundi lake walidai kwamba ripoti ya BBI itahujumu hatua muhimu ambazo zimeafikiwa katika katiba ya Kenya.

Lakini Nzibo kwa upande wake alipuuzilia mbali taarifa ya Naado akisema kwamba huo ulikuwa msimamo wake wa kibinafsi.

“Hayakuwa maoni ya wailslamu. Hawakushauriana na waislamu, kwa hivyo yalikuwa maoni ya kibinafsi,” Nzibo alisema.

View Comments