In Summary
  • Rais Samia Suluhu Hassan ampendekeza Philip Isdory Mpango kuwa makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
  • Baada ya kupokea Spika Job Ndugai alilitangazia bunge hilo jina hilo lililopendekezwa na Rais Samia
Rais mpya wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Rais Samia Suluhu Hassan ampendekeza Philip Isdory Mpango kuwa makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jina hilo liliwasilishwa bungeni asubuhi ya Jumanne na mpambe wa rais katika bahasha maalum.

Baada ya kupokea Spika Job Ndugai alilitangazia bunge hilo jina hilo lililopendekezwa na Rais Samia.

Mara baada ya tangazo hilo bunge lililipuka kwa shangwe.

Bwana Mpango amekuwa waziri mwandamizi katika serikali ya hayati John Magufuli akihudumu kama waziri wa fedha.

Kwa sasa, bunge la Tanzania linatarajiwa kupiga kura ili kuthibitisha uteuzi huo wa Mpango.

Na kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, asilimia 50 ya wabunge wanatakiwa kuukubali uteuzi huo ili kuthibitishwa.

Kabla ya jina hilo kuwasilishwa bungeni hii leo, kwanza liliwasilishwa katika Kamati kuu ya chama tawala CCM na kuthibitishwa.

Mara tu baada ya jina lake kusomwa Spika Ndugai alimpatia Mpango muda wa kujieleza ndani ya Bunge.

Mpango akaeleza kuwa hakujua chochote juu ya uteuzi huo na kwamba alipigwa na butwaa.

''...Hii ni heshima kubwa sana, sikuwahi kuota (kama nitaipata)...Mpaka Naibu Waziri wangu akiwa anajibu maswali asubuhi hapa, nilikuwa nafikiria majukumu yangu yanayonikabili ikiwemo mishahara ya wabunge ambayo baadhi imechelewa mpaka asubuhi hii. Nipepigwa na butwaa..."

Dkt. Philip Mpango amekua Waziri wa Fedha na Mipango katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Magufuli.

Mwaka 2015 Alikua mbunge wa kuteuliwa.

Bwana Mpango ni mzaliwa wa Kigoma, baba yake ni marehemu Isidori Nzabhayanga Mpango, ambaye alizaliwa Kijiji cha Kasumo, Wilaya ya Kasulu.

Dkt. Mpango alizaliwa hapohapo Kasumo na ni kaka mdogo wa Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanganyika Magharibi - Kasulu mkoani Kigoma, Dk Gerard Mpango.

Dk Mpango ni mchumi mwenye shahada ya uzamivu ya uchumi.

Kuanzia miaka ya 1990 hadi 2000, alifanya kazi akiwa mhadhiri mwandamizi wa uchumi katika kitivo cha Biashara (sasa Shule ya Biashara) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

 

 

 

Rais mpya wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
View Comments