In Summary
  • Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo amefanya mabadiliko ya Wakuu wa mikoa, huku wengi wao wakihamishiwa katika mikoa mipya na wengine wakistaafu 
rais samia suluhu. Picha: BBC

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo amefanya mabadiliko ya Wakuu wa mikoa, huku wengi wao wakihamishiwa katika mikoa mipya na wengine wakistaafu utumishi wa umma.

Taarifa ya uteuzi wa wakuu hao wa taasisi pamoja na wakuu wa mikoa ulioanza leo Jumamosi Mei 15, 2021 imetolewa leo na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu, Gerson Msigwa, ikieleza kuwa wataapishwa Mei 18, 2021 Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Rais Samia ameingiza sura chache mpya katika ngazi hiyo ya utawala, akiwemo aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais kutoka upinzani Queen Sendiga na Amos Makalla ambaye anarejea tena uongozini baada ya miaka mingi.

Wengi miongoni mwa wale walioachwa nje ya orodha ndefu ya watu 45 ni 10 na wanasemekana kuwa wamefikisha umri wa kustaafu, na wanajumuisha mwanamke mmoja kutoka upinzani mama Mgwira.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Mkurugenzi wa mawasiliano ya Ikulu Gerson Msigwa, Rais Samia amewateua Amos Gabriel Makalla kama mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam akichukua nafasi ya Abubakar kunenge ambaye amehamishiwa Pwani.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Bwana Amos Makalla kuhudumu kama Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam baada ya kuchaguliwa awali kabla ya kuteuliwa kama Waziri wa michezo wakati wa utawala wa rais Jakaya Kikwete.

Anthony John Mtaka anachukua nafasi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma mjini , na kabla ya uteuzi huu alikuwa Simiyu huku Albert Chalamila akihamishwa kutoka Mbeya na kwenda Mwanza kuchukua nafasi ya John mongella ambaye amehamishiwa Simiyu.

David Zacharia Kafulila anakuwa Mkuu mpya wa mkoa wa Arusha akichukua nafasi ya Iddi Hassan Kimante ambaye amestaafu.

Steven Kagaigai anakwenda kuwa Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, na kabla alikuwa katibu wa bunge, akichukua nafasi ya Anna Elisha Mghwira ambaye amestaafu.

Adam Kigoma Malima ambaye alikuwa zamani Mkuu wa mkoa wa Mara , anachukua nafasi ya Martin Reuben Shigella katika mkoa wa Tanga, Shigella ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro .

Juma Zuberi Homera ambaye alikuwa Mkuu wa mkoa wa Katavi anachukua nafasi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya, kutoka kwa Albert Chalamila.

Aidha , Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kwa sasa yuko Zanzibar amemteua mwanae rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere, Makongoro Nyerere kama Mkuu wa mkoa wa Manyara akichukua nafasi ya Mkirikiti ambaye amepelekwa Rukwa.

Mkuu wa mkoa pekee aliyesalia kwenye mkoa wake katika mabadiliko haya ni mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye.

Rais Samia Suluhu Hassan pia amefanya uteuzi wa watendaji wakuu wa taasisi za Serikali akiwemo mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni kuchukua nafasi ya Brigedia Jenerali John Mbungo atakayepangiwa kazi

Mbali na Hamduni ambaye amepandishwa cheo kuwa kamishna wa polisi kutoka kamishna msaidizi wa polisi, amemteua Sylvester Mwakitalu kuwa mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kuchukua nafasi ya Biswalo Mganga ambaye ameteuliwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu.

 

 

 

View Comments