In Summary
  • Tanzania yazindua mtambo mkubwa zaidi Afrika Mashariki wa kusafisha dhahabu

Rais wa Tanzania Bi. Samia Suluhu amezindua leo kiwanda cha kusafisha dhahabu jijini Mwanza kinachoitwa Mwanza Precious Metals Refinery.

Kiwanda hicho chenye thamani ys Bilioni 12.2 za Kitanzania sawa na dola za Kimarekani milioni 5.2 katika uwekezaji wake kitasafisha dhahabu yote ya Tanzania.

Aidha kiwanda hiki kinatajwa kuwa kikubwa zaidi kuliko vyote Afrika Mashariki na kazi yake kubwa itakuwa kusafisha dhahabu za kimataifa.

Kwa siku moja kiwanda kina uwezo wa kusafirisha dhahabu kilo 480 na zinaweza kuongezeka mpaka kufika kilo 960 kwa siku katika kiwango cha juu kabisa cha kimataifa, yaani dhahabu ya Tanzania itasafishwa kwa asilimia 99. 9 ambayo ni karibu 100% .

Katika uzinduzi wa kiwanda hicho, Rais Samia amesema ameona kiwanda hicho kuwa cha miujiza wakati alipoingia ndani kukiona. "Nimeoneshwa vigololi vya dhahabu. Vimeingizwa kwenye mitambo ni dakika 3 kama zilitimia, tayari imeshayeyushwa imetengenezwa bar. Kwahiyo ni mtambo ambao ni wa kisasa wa hali ya juu. Wasiwasi wangu upo kwenye upatikanaji wa malighafi kama kwa siku ni kilo 480 ingawa kuna mashine ndogo ambazo zinasafisha kilo 80 kwa siku nadhani ni kuendana na upatikanaji wa malighafi."

Aidha aliongeza kusema kuwa jukumu la serikali sasa ni kuweka sera, sheria ambazo zitawawezesha wachimbaji wachimbe zaidi malighafi ipatikane kwa wingi zaidi.

Hata hivyo Rais Samia ametoa wito kwa wachimbaji kutumia fursa hii wakati serikali ikiendelea kuimarisha sekta hii ya madini ikiwemo kudhitibi wizi, utoroshaji na biashara ya magendo ya rasilimali zetu za madini, na moja wapo ya maeneo ambayo mnatakiwa kuimarisha ni mgodi wetu wa Tanzanite.

"Kama tunavyojua Mungu aliipendelea nchi yetu Tanzania peke yake dunia nzima. Ni madini yanayopatikana Tanzania peke yake dunia nzima lakini tunavyokwenda sasa ni kama madini yanayochimbwa dunia nzima. Ukienda kwa majirani zetu kuna Tanzanite nyingi tu.

Kuna haja ya kukaa kuitangaza Tanzanite yetu, kuna haja ya kuipa jina ambayo itaipa umuhimu na upekee Tanzanite yetu, lakini pia kuna haja ya kuwa na mfumo wa kuidhibiti. Kuwe na mashirika ambayo yataidhibiti Tanzanite yetu ili kuwe na mwamvuli mmoja wa kununua Tanzanite yetu. Kwahiyo, nakuomba Waziri kaa na Wawekezaji mtengeneze mfumo ambao utailinda Tanzanite yetu. Nasemea Tanzanite kwa sababu ndio zao pekee na madini pakee tuliyonayo ambayo tunaweza kuweka jina letu pale".

Pia rais ametaka marekebisho yafanyike katika kutoza kodi , Rais Samia amesema VAT kwa madini yanayoletwa kutoka nje idaiwe baada ya kuchenjua, wanaoleta madini kutoka nchi jirani walete yasafishwe halafu kodi zitapatikana baada ya kusafisha malighafi za madini.

 

 

 

View Comments