In Summary
  • Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo
  • Kundi hilo liliwalenga jamii ya wachache wa dhehebu la Shia hapo awali, huku wauaji wa kujitolea muhanga wakishambulia misikiti , klabu za michezo na shule
Shambulio baya lakumba msikiti wa Kunduz wakati wa ibada ya Ijumaa
Image: BBC

Mlipuaji wa kujitolea muhanga amelenga msikiti mmoja kaskazini mwa mji wa Afghanistan wa Kunduz wakati wa ibada ya Ijumaa na kuwaua takriban watu 50.

Picha katika mitandao ya Kijamii zimeonesha miili na vifusi ndani ya msikiti , unaotumika sana na jamii ya walio wachache wa dhehebu la Shia.

Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo.

Waislamu wenye itikadi kali wa dhehebu la Sunni ikiwemo kundi la wapiganaji wa Islamic State, wamelenga jamii ya Washia kwasababu wanawachukulia kuwa watu wazushi.

Tawi la IS-K la kundi la IS nchini Afghan ambalo linapinga kundi la wapiganaji wa Taliban, limetekeleza mashambulizi kadhaa ya mabomu hivi majuzi likilenga eneo la mashariki mwa taifa hilo.

Mfanyabiashara wa eneo hilo Zalmai Alokzai, ambaye alikimbia hadi katika hospitali kutazama iwapo madaktari walihitaji damu, alielezea kuona picha za kutisha.

''Ambyulansi zilikuwa zikienda na kurudi katika eneo la shambulio hilo kubeba miili', aliambia chombo cha habari cha AFP

Huku kukiwa hakuna ambaye ametangaza kuhusika na shambulio hilo kufikia sasa, shambulio hilo lina dalili za ;kutekelezwa na IS-K , kundi lililoshambulia uwanja wa ndege wa Kabul mwezi Agosti.

Kundi hilo liliwalenga jamii ya wachache wa dhehebu la Shia hapo awali, huku wauaji wa kujitolea muhanga wakishambulia misikiti , klabu za michezo na shule.

Katika wiki za hivi karibuni, kundi la wapiganaji wa IS limeanzisha kampeni ya mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa kundi la Taliban.

Kundi la IS lilishambulia ibada ya wafu iliohudhuriwa na idadi kubwa ya viongozi wakuu wa Taliban mjini Kabul siku ya Jumapili, na kumekuwa na msururu wa mashambulizi madogo katika mkoa wa mashariki wa Nangarhar na kunar, ambapo IS ilikuwa na ngome yake.

Mashambulizi ya Ijumaa iwapo yalitekelezwa na kundi la wapiganaji wa IS , yataidhinisha upanuzi wa vitendo vyake katika eneo la kaskazini la taifa hilo.

Taliban inasema kwamba imewakamata makumi ya wanachama wa kundi la IS na wanaaminika kuwaua wengine wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na kundi hilo, lakini pia wamepuuza tisho la IS.

Raia wengi wa Afghanistan walitumai kwamba ujio wa utawala wa Taliban nchini Afghanistan ungeleta amani badala ya uongozi wa kiimla.

Lakini IS inawakilisha tishio kubwa kwa ahadi zake za kuimarisha usalama.

Taliban ilichukuwa udhibiti wa Afghanistan baada ya wanajeshi wa kigeni kuondoka nchini humo mwezi Agosti kufuatia makubaliano kati ya Marekani na Taliban , miongo miwili baada vikosi vya Marekani kuwaondoa wapiganaji hao katika mamlaka 2001.

 

 

View Comments