In Summary
  • Serikali ya Tanzania imetangaza rasmi kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa kwasababu ya kupata ujauzito wakiwa shuleni kurejea masomoni kupitia mfumo rasmi
Pregnant Student
Image: FILE

Serikali ya Tanzania imetangaza rasmi kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa kwasababu ya kupata ujauzito wakiwa shuleni kurejea masomoni kupitia mfumo rasmi.

Uamuzi huo umetangazwa leo na waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia , Profesa Joyce Ndalichako alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusu mafanikio ya wizara hiyo katika miaka 60 ya uhuru wa Taifa hilo.

Mbali na wanafunzi waliopata mimba, wanafunzi wengine waliokatiza masomo ya kwa sababu mbalimbali nao wataruhusiwa kurejea katika mfumo huo rasmi.

'Takwimu za elimu zinaonyesha kwamba wanafunzi wanaacha shule kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utoro, ujauzito, vifo pamoja na nidhamu, lakini sababu kubwa katika takwimu za utoro shuleni ambapo kwenye shule za msingi ni 100,008 ambapo wanafunzi watoro ni asilimia 93%, mimba ni asilimia ndogo tu, takribani asilimia 5% ya wanafunzi wanaoacha shule, alisema waziri Ndalichako.

Kwa mujibu wa Waziri Ndalichako wanafunzi watakaotaka kurejea shule wataruhusiwa kufanya hivyo ndani ya miaka miwili baada ya kuwa nje ya mfumo rasmi kwa utoro ama kukatiza masomo.

'yule ambaye matatizo yaliyomsababisha atoke shuleni yatakuwa yamekwisha na anataka kurudi shuleni serikali itampa nafasi na itakuwa ndani ya miaka miwili tangu alipoacha shule', alisema

Mwezi Juni mwaka huu akizungumza na wakuu wa vyuo vya maendeleo ya wananchi nchini humo, Katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo aligusia kurejea masomoni kwa wanafunzi hao kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi.

Akawataka wakuu hao wa vyuo kuhakikisha kuwa wanafunzi wa kike walioshindwa kuendelea na masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba wanarudi na kuendelea na masomo.

Pamoja na hatua hii ya wakati huo, kupongezwa lakini bado haikuwafurahisha zaidi wanaharakati wa elimu waliotaka wanafunzi hao kurejea kwenye mfumo ramsi.

Tamko jipya la sasa la Serikali ya Tazanzania kuruhusu wanafunzi waliopata mimba na changamoto zingine kurejea masomoni linahitimisha marufuku iliyodumu kwa zaidi ya miaka minne iliyowekwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, hayati John Pombe Magufuli.

Juni 2017 Hayati Magufuli alipiga marufuku wanafunzi wanaopata mimba mashuleni kuendelea na masomo ya shule ya msingi na sekondari akisema ndani ya utawala wake hakuna mwanafunzi atakayepata mimba na kuruhusiwa kurudi shuleni.

Akazitaka taasisi zinazotetea utaratibu wa wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni, kufungua shule zao za wazazi lakini si kuilazimisha Serikali kufanya hivyo.

Kauli ya Magufuli ikazua mijadala na upinzani kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu nchini na nje ya nchi hiyo, wakiona hatua hiyo ni kumnyika haki ya kupata elimu mtoto wa kike.

Shirika la Human Rights Watch lilisema mwezi uliopita kwamba marufuku hiyo ya serikali ya Tanzania kwa wanafunzi waliopata mimba imewanyima maelfu ya wasichana haki ya kupata elimu.

Shirika hilo lilisema liliwahoji wasichana na wanawake 30 wenye kati ya umri wa miaka 16 na 24 kuju walivyoathirika, wote walikuwa wamefukuzwa shuleni au kukoma kwenda shule za msingi au sekondari kati ya mwaka 2013 na 2021 kwa ajili ya ujauzito.

Tanzania ina rekodi isiyofurahisha ya wasichana wadogo kupata mimba. Mimba za utotoni ni tatizo lililowakumba asilimia 22 ya mabinti wenye umri kati ya miaka 20 mpaka 24 walipata watoto kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Kwa mujibu wa Shirika linaloshughulikia haki za wanawake la Center for Reproduction Rights, kati ya mwaka 2003 na 2011, zaidi ya mabinti 55,000 walilazimika kuacha shule huku wengine wakifukuzwa kwa sababu ya kupata mimba mashuleni.

Kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kupata ujauzito, kulimsukuma Rais wa wakati huo, Marehemu Magufuli kutaka wanafunzi hao kutoendelea na masomo.

 

 

View Comments