In Summary

•Chanzo cha moto huo hakijajulikana, lakini inadhaniwa kemikali zilihifadhiwa katika baadhi ya makontena.

•Wengi wa waliojeruhiwa wanaripotiwa kuwa katika hali mbaya huku majeraha ya moto yakichukua asilimia 60 hadi 90 ya miili yao.

Image: BBC

Moto na mlipuko mkubwa umesababisha vifo vya takriban watu 40 baada ya vifo 8 kuongezeka na mamia ya wengine kujeruhiwa kwenye ghala moja lililoko karibu na mji wa Chittagong, Bangladesh.

Mamia ya watu walifika kukabiliana na moto huo wakati makontena kadhaa yalilipuka katika eneo la Sitakunda. Chanzo cha moto huo hakijajulikana, lakini inadhaniwa kemikali zilihifadhiwa katika baadhi ya makontena hayo. Hospitali katika eneo hilo zimezidiwa na zimeomba kuchangia damu. Wengi wa waliojeruhiwa wanaripotiwa kuwa katika hali mbaya huku majeraha ya moto yakichukua asilimia 60 hadi 90 ya miili yao.

"Mlipuko huo ulinirusha umbali wa mita 10 kutoka mahali nilipokuwa nimesimama. Mikono na miguu yangu imeungua," dereva wa lori Tofael Ahmed aliambia shirika la habari la AFP.

Mhudumu mwingine wa kujitolea aliambia shirika hilo kuwa ameona miili zaidi ndani ya eneo lililoathiriwa na moto huo. Wazima moto kadhaa ni miongoni mwa waliouawa na kujeruhiwa. Bohari hiyo ilikuwa na nguo za mamilioni ya dola zilizokuwa zikisubiri kusafirishwa kwa wauzaji reja reja wa nchi za Magharibi, kulingana na afisa wa serikali ya eneo hilo. Bangladesh ni muuzaji mkuu wa nguo kwa nchi za Magharibi.

View Comments