In Summary

•Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padre Charles Kitima amesema kuwa Kanisa litatoa ushirikiano ili haki ipatikane katika kesi hiyo.

•Padre Kitima amesema kuwa wanalichukulia suala hili kama jambo baya kwa sababu linasababisha mashaka makubwa kwa wazazi na watoto, 

Korokoroni
Image: BBC

Padri wa Kanisa Katoliki Kaskazini mwa Tanzania, amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kudhalilisha watoto kingono, polisi imethibitisha.

Watoto hao ni wanafunzi wa kuanzia darasa la sita hadi kidato cha kwanza waliokuwa wakihudhuria mafundisho ya komunio ya kwanza na kipaimara.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padre Charles Kitima amesema kuwa Kanisa litatoa ushirikiano ili haki ipatikane katika kesi hiyo.

‘’Tunasema kuwa tunasubiri maamuzi hayo [ya mahakama] ambayo yatasababisha maamuzi mengine kufanywa… lazima kuthibitisha  na yeye lazima apewe haki ya kujitetea  hilo ndilo linalosubiriwa,’’ amesema Kitima

‘’Mkondo wa sheria utachukua utaratibu wake na kanisa litatoa ushirikiano ili kuhakikisha kwamba waliokosewa haki zao wametendewa haki’’

Msimamo wa Kanisa Katoliki

Padri Kitima ameileza BBC kuwa kwa ujumla wake Kanisa Katoliki linapingana na vitendo vya udhalilishaji kingono kwa watoto kwa kuwa kanisa linatakiwa sehemu salama kwa woatu wote. 

‘’Tukiri kwamba hili ni tatizo ambalo ni tabia ya mtu husika, tuna mapadri zaidi ya 3000 nchini hapa lakini unapata sasa katika hao, unakuta hao wenye madhaifu na mapungufu ndiyo inakuwa hivyo’’.

Padre Kitima amesema kuwa wanalichukulia suala hili kama jambo baya kwa sababu linasababisha mashaka makubwa kwa wazazi na watoto, watoto wanapokwenda kwenye shughuli kama hizo wana matumaini kwamba wanapata mtu anayewalea kiroho.

‘’Wanapofanyiwa vitu ambavyo ni kinyume na waliyoyaendea yanakuwa masikitiko makubwa’’.

‘’Sisi kama Kanisa tunasikitika kwa tabia mbaya za mtu mmoja mmoja ambazo zinaenda kinyume na kile ambacho tunategemewa kukijenga,kujenga mtu katika maadili mazuri’’.

Padre Kitima amesema duniani watu kama hao wapo na kama jamii ni muhimu kushirikiana katika kubadili mienendo na kuona namna  ya kutoa taarifa linapokuwepo hili suala na linapobainika.

Utoaji taarifa kuhusu matukio ya udhalilishaji yanapotokea

Padri Kitima amesema kuwa utaratibu wa utoaji taarifa uko bayana katika kanisa, kuanzia kwenye Baraza la Maaskofu  kamati yenye watu waliobobea katika kushughulikia masuala hayo.

‘’Taarifa ya kwanza baada ya kujiridhisha kwamba kuna tatizo hata kama tetesi kwamba kuna udhalilishaji kwa watoto unatoa taarifa kwa mkubwa wa huyo, kama ni padre unatoa taarifa kwa Askofu wa jimbo lake. Kama ni Katekista aliyekuwa anafundisha dini,au ni mzazi aliyepewa jukumu na kanisa kutoa huduma, taarifa zinatolewa kwa Paroko’’.

‘’Nje ya kuwa suala hili ni dhambi na chukizo kwa Mwenyezi Mungu lakini lina madhara kwa watoto hivyo ni lazima lichukuliwe hatua za kisheria za nchi,’’ amesema Padre Kitima.

View Comments