Raia wa jamii wa Maasai Loliondo
Image: BBC

Mahakama ya Afrika mashariki imetupilia mbali shauri lilofunguliwa na jamii ya wamaasai kupinga kuondolewa kwenye eneo wanalodai kuwa ni ardhi yao ya asili

Kwa mujibu wa Majaji waliokuwa wanasikiliza shauri hilo, Jaji Charles Nyachaekwa kwa niaba ya Jaji Monica Mugenyi amesema waleta maombi hawakuwasilisha Ushahidi wa kutosheleza kuithibitishia mahakama hiyo bila shaka kuwa kulikuwa na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa mkataba wa Afrika mashariki.

Katika utetezi wake serikali ya Tanzania kupitia mwasheria mkuu wa serikali alieleza kwamba zoezi lilotekelezwa na serikali ni kuwaondoa wafugaji waliovamia eneo hilo la pori tengefu linalopakana na hifadhi ya taifa ya Serengeti na Ngorongoro kwa kutambua umuhimu wa eneo katika uhifadhi wa Wanyama pori kutokana na kutumika kama mazalia kwa Wanyama hao na kuwa na vyanzo vingi vya maji ambavyo vinahudumia hifadhi hizo.

Mawakili waliokuwa wanawakilsha jamii hiyo wamesema watakata rufaa kupinga maamuzi hayo yaliyoupa upande wa serikali ushindi

“Kama mawakili wa walalamishi hatujafurahishwa na maamuzi ya mahakama, hatujakata tamaa tutaongea na wateja wetu nao wasikate tamaa bado hatujamaliza safari” - Ester Mnaro wakili wa upande wa waleta maombi.

Kwa upande wa wawakilishi wa jamii hiyo waliokuwepo mahakamani hapo wameeleza kusikitishwa kwao na maamuzi hayo ya mahakama.

Isaya Laizer anasema mahakama hiyo ingeona utu kwa jamii hiyo kutokana na kuendelea kukiukwa kwa haki yao tangu mwaka 2017 licha ya kuweko kwa zuio la mahakama serikali iliendesha operesheni

Neema Mollel – “Majibu ambayo yametolewa yametukatisha tamaa kabisa lakini hatutakata tamaa tutakata rufaa na tuko tayari kwenda mbele zaidi”

Mwezi june mwaka huu kuliibuka makabiliano baina ya polisi na raia kwenye eneo hilo la Loliondo na kupelekea kifo cha askari mmoja wakati wa uwekaji mipaka kutenga kilomita za mraba 1500 kwa ajili ya uwindaji na mazalia ya wanyama pori.

Kwa mujibu wa ripoti za watetezi wa haki za binadamu mamia ya wakazi wa eneo hilo walikimbia makazi yao huku baadhi wakikimbilia taifa Jirani la Kenya kusaka hifadhi na matatibabu kwa wale ambao walijeruhiwa wakati wa makabiliano ambayo serikali iliyakanusha

View Comments