In Summary

•Imedaiwa wafungwa 4,000 walioachiwa huru kwa msamaha wa rais Mnangagwa wiki iliyopita wanajumuisha wabakaji watoto.

•Baadhi ya Wazimbabwe kwenye mitandao ya kijamii pia wametaka uamuzi huo kubatilishwa kwani unawaweka wanawake katika hatari.

Image: BBC

Muungano wa upinzani nchini Zimbabwe Citizens Coalition for Change (CCC) umedai kuwa zaidi ya wafungwa 4,000 walioachiwa huru kwa msamaha wa rais wiki iliyopita wanajumuisha wabakaji watoto.

Rais Emmerson Mnangagwa aliwasamehe wafungwa waliotoka katika magereza 47 ya nchi hiyo katika jaribio la kupunguza msongamano.

Mamlaka za magereza hata hivyo zilisema, ubakaji ni miongoni mwa makosa ambayo hayakujumuishwa katika msamaha huo.

Video zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha kile ambacho vyombo vya habari vya nchini humo vilisema ni wabakaji wakisherehekea uhuru wao huku baadhi yao wakisemekana kuwa wametumikia hukumu yao kwa chini ya mwaka mmoja.

CCC katika taarifa yake siku ya Jumatano ilisema "haikuwa sawa kuwaachilia wahalifu hatari na ambao hawajarekebishwa kujumuika tena na jamii" kabla ya kuwaarifu au kuwatayarisha kisaikolojia waathiriwa wa ubakaji.

"Kumwachilia mbakaji ambaye hajarekebisha maadili yake katika jamii bila ulinzi wowote wa kuwalinda waathiriwa kunahatarisha wanawake na wasichana na kamwe hakuwezi kuwa na sababu za msingi katika jamii ya kidemokrasia," msemaji wa CCC Fadzayi Mahere alisema.

Baadhi ya Wazimbabwe kwenye mitandao ya kijamii pia wametaka uamuzi huo kubatilishwa kwani unawaweka wanawake katika hatari.

Mwanahabari mashuhuri wa uchunguzi Hopewell Chin’ono alisema msamaha "kamwe hautolewi kwa wabakaji au watu ambao wamefanya uhalifu wa kikatili".

Bw Chin’ono, mkosoaji wa serikali, alisema wanawake wa Zimbabwe hawatakuwa salama kufuatia msamaha huo.

Mamlaka za Zimbabwe bado hazijatoa maoni yoyote kuhusu madai hayo.

View Comments