In Summary

• Al-Shabab walisema wameteka kambi hiyo na kuua makumi ya wanajeshi wa ATMIS, lakini madai hayo hayajathibitishwa.

Kundi la al-Shabab leo Ijumaa asubuhi lilifanya shambulizi dhidi ya kituo cha wanajeshi wa Uganda cha Kikosi Umoja wa Afrika (ATMIS) katika wilaya ya Bulla Mareer, eneo la Lower Shabelle nchini Somalia.

Shambulio hilo lilianza muda mfupi baada ya sala ya asubuhi.

Lilianza na mlipuko mkubwa, unaoaminika kuwa gari la vilipuzi.

Buulo Mareer iko takriban kilomita 110 kutoka mji mkuu, Mogadishu.

Wakazi waliripoti kuwa baada ya mlipuko huo mkubwa, milipuko miwili zaidi ilisikika katika kambi hiyo, kabla ya mapigano kuanza kati ya wanajeshi wa Uganda na washambuliaji

Al-Shabab walisema wameteka kambi hiyo na kuua makumi ya wanajeshi wa ATMIS, lakini madai hayo hayajathibitishwa.

ATMIS inasema vikosi vyake kwa sasa vinatathmini hali ya usalama katika eneo hilo lakini hakuna kauli iliyotolewa na serikali ya Somalia kuhusiana na shambulio hilo.

Msemaji wa jeshi la Uganda Felix Kulayigye ameliambia gazeti la Daily Nation la Kenya kwamba wanajeshi wanachunguza shambulio hilo.

Aliwalaumu "waasi wa kigeni" kwa uvamizi huo bila kutoa maelezo zaidi.

Kiwango cha uharibifu uliosababishwa na shambulio hilo bado hakijajulikana.

Raia wamesalia ndani ya nyumba zao na licha ya baadhi ya risasi zilizofyatuliwa kugonga nyumba zao, hakuna uharibifu ulioripotiwa.

Baadhi ya wakazi wa Bulo Mareer waliambia BBC kwamba walisikia sauti za helikopta zikipaa juu ya jiji hilo.

View Comments