In Summary

•Wawili hao wamepatikana na hatia ya uoga wakati wapiganaji wa Kiislamu walipovamia kambi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia mwezi Mei.

•Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alikosoa jeshi lake kwa namna lilivyojibu shambulio hilo.

Kikosi cha wanajeshi 19,000 wa Umoja wa Afrika kinatarajiwa kuondoka Somalia mwaka ujao (picha maktaba)
Image: BBC

Mahakama ya kijeshi nchini Uganda imewapata maafisa wawili na hatia ya uoga wakati wapiganaji wa Kiislamu walipovamia kambi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia mwezi Mei.

Meja Zadock Abor na John Oluka walikimbia baada ya kushambuliwa na al-Shabab huko Bulo Marer, kusini mwa mji mkuu Mogadishu.

Takriban wanajeshi 50 wa Uganda waliuawa, maafisa wanasema.

Uganda ni sehemu ya kikosi cha Umoja wa Afrika kinachoisaidia serikali ya Somalia kupambana na al-Shabab, tawi la al-Qaeda.

Shambulio dhidi ya Bulo Marer lilikuwa moja ya mauaji mabaya zaidi kwa kikosi cha Umoja wa Afrika, Atmis, tangu kilipoanzisha mashambulizi mapya dhidi ya al-Shabab mwaka jana.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alikosoa jeshi lake kwa namna lilivyojibu shambulio hilo.

Mahakama ya kijeshi ya Uganda iliyoketi mjini Mogadishu ilisikia kwamba maafisa hao walikuwa wamepewa onyo kuhusu shambulio lililokuwa likikaribia lakini walishindwa kuchukua hatua za kulizuia.

Wanamgambo wa al-Shabab walipovamia kambi hiyo, walishindwa kuwakusanya wanajeshi wao na badala yake walikimbilia kambi nyingine.

Maafisa wote wawili wamefutwa kazi katika jeshi.

Wanajeshi wengine wanne pia walipatikana na hatia ya kushindwa kulinda zana za kijeshi.

Kikosi cha wanajeshi 19,000 wa Umoja wa Afrika kilitumwa Somalia mwaka 2007 na kusaidia kuwaondoa al-Shabab katika miji mingi.

Imepangwa kuwa kikosi hicho kitarejesha majukumu ya usalama kwa vikosi vya serikali ya Somalia na kuondoka nchini mwaka ujao.

Hata hivyo, mashambulizi dhidi ya al-Shabab yamekwama na kundi hilo bado linadhibiti maeneo mengi ya vijijini nchini humo.

View Comments