In Summary

• Wawili hao wanadaiwa kuomba kulipwa Shilingi milioni 2.5 za Uganda kutoka kwa jamaa za washukiwa.

Mahakama
Image: MAHAKAMA

Hakimu mkuu nchini Uganda aliyekamatwa kwa tuhuma za ufisadi alizua kizaazaa katika mahakama ya mjini Kampala baada ya kuanza kupiga nduru akilia na kujigaragaza sakafuni.

Kwa mujibu wa jarida la Independent, hakimu mkuu huyo, Sylvia Nvanungi, ni wa mahakama ya Mitooma na baada ya kisanga hicho, aliwekwa kwenye rumande na mwenzake, Wakili wa Serikali Mkazi wa Sembabule, Jacqueline Bako, kwa tuhuma za rushwa.

Wawili hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi Joan Aciro ambaye aliwashtaki kwa makosa manane ya ufisadi.

Bako alihusishwa na mashtaka yote, huku Nvanungi akihusishwa katika shtaka moja. Makosa haya yanadaiwa kutokea wakati Nvanungi akiwa Hakimu Mkuu wa Sembabule mapema mwaka huu.

Mahakama ilisikiza kuwa Aprili 2023, wakiwa kwenye nyadhifa za umma, wawili hao wanadaiwa kuomba kulipwa Shilingi milioni 2.5 za Uganda kutoka kwa jamaa za washukiwa.

Kiasi hiki kiliripotiwa kubadilishwa kwa dhamana au kubadilisha karatasi za mashtaka. Upande wa mashtaka unadai kuwa Bako alipokea Shilingi milioni 1.48 kutoka kwa Franco Mulangwa kama sehemu ya utaratibu huu.

Mashtaka hayo pia ni pamoja na mashtaka dhidi ya Bako ya kuomba na kupokea fedha kutoka kwa watu mbalimbali kwa ajili ya fadhila zinazohusiana na dhamana na kubadilisha mashtaka ya kisheria.

Mshtakiwa alikana mashitaka hayo na kuomba apewe dhamana. Mahakama ilikataa ombi lao kwa sababu ya ukosefu wa wadhamini wa kuaminika.

Nvanungi alitoa hoja ya kuachiliwa kwake kutokana na masuala ya afya binafsi na majukumu ya kifamilia, akitolea mfano haja ya kueleza hali yake kwa mamlaka za mahakama.

Licha ya ombi lake la kihisia, mahakama ilimnyima dhamana kwa kuzingatia uhaba wa nyaraka zilizotolewa na wadhamini waliopendekezwa.

View Comments