In Summary

• Uchimbaji madini usiodhibitiwa na ulio kinyume cha sheria ni jambo la kawaida nchini Tanzania.

Image: Getty Images

Watu 22 wamefariki dunia kufuatia maporomoko ya udongo katika mgodi kaskazini mwa Tanzania, Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan amesema.

Rais Hassan alisema maporomoko hayo yametokea katika mgodi wa Ng'alita wilayani Bariadi, mkoani Simiyu.

“Watanzania wenzetu hawa walikuwa wachimbaji wadogo katika eneo hilo, wakijaribu kujitafutia riziki wao wenyewe na familia zao,” Rais Hassan alisema.

Mashirika ya ulinzi yanajitahidi kuondoa miili zaidi kutoka kwa vifusi, alisema.

“Awali tuliambiwa kulikuwa na watu 19 hadi 20 waliokuwa wamenaswa migodini lakini kwa bahati mbaya tukaishia kuopoa miili 22,” Simon Simalenga, mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani humo, aliliambia shirika la habari la Reuters.

Alisema kundi hilo la watu lilianza kuchimba madini katika eneo hilo lenye madini mengi takriban wiki tatu zilizopita kabla ya serikali kuleta taratibu za usalama.

Eneo hilo lilizuiwa kwa sababu ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

“Afisa madini wa mkoa aliwatembelea na kuwazuia kuchimba madini kwa kuwa ilikuwa inafanyia kazi taratibu zinazotakiwa” Bw Simalenga alisema.

Uchimbaji madini usiodhibitiwa na ulio kinyume cha sheria ni jambo la kawaida nchini Tanzania, ambayo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu duniani.

View Comments