In Summary

•Tukio la Ijumaa lilikusudiwa kuwa harusi ya pamoja lakini Waziri Kennedy-Ohanenye aliwasilisha agizo la mahakama kuikomesha.

•Waziri Kennedy-Ohanenye alisema angewatunuku biharusi wote ufadhili wa masomo na malipo ya kila mwezi kwa miezi sita ya kwanza ya ndoa zao.

Image: BBC

Takriban wasichana 100 miongoni mwao yatima kadhaa wameolewa katika sherehe tofauti nchini Nigeria licha ya mpango huo kuzua gumzo kali nchini humo.

Tukio la Ijumaa lilikusudiwa kuwa harusi ya pamoja lakini Waziri wa Masuala ya Wanawake Uju Kennedy-Ohanenye aliwasilisha agizo la mahakama kuikomesha, akihofia kuwa baadhi ya wasichana walikuwa na umri mdogo.

Alirejea uamuzi huo baada ya kufikia makubaliano na Spika wa Bunge la Jimbo la Niger, Abdulmalik Sarkin-Daji, ambaye aliunga mkono harusi hiyo ya halaiki, kwa wasichana hao kuwa na sherehe za kibinafsi.

"Sikuwa na nia ya kusitisha ndoa hiyo lakini kuhakikisha wasichana wamefikia umri wa kuolewa na hawakulazimishwa," Bi Kennedy-Ohanenye alisema katika taarifa.

BBC inaelewa kuwa sharti la sherehe hizo kuendelea ni kwamba wanawake wote waliohusika walipaswa kuwa na umri wa kisheria, ambao ni 18 nchini Nigeria.

Waziri Kennedy-Ohanenye alisema angewatunuku biharusi wote ufadhili wa masomo na malipo ya kila mwezi kwa miezi sita ya kwanza ya ndoa zao.

Mmoja wa wazazi wa maharusi hao, Mallama Amina Mariga, aliiambia BBC kuwa harusi hiyo ya pamojai ilipangwa ili "kuwasherehekea wasichana hao kwa usawa na kuwapa hisia ya umoja".

Bi Mariga, kama familia nyingi, alipewa vitu kwa ajili ya harusi ya bintiye na malipo ya mahari, ikiwa ni pamoja na kitanda na cherehani kutoka kwa wanasiasa.

Wengi wa wanawake vijana wamepoteza jamaa zao kutokana na mashambulizi ya majambazi wenye silaha, ambao mara kwa mara huwalenga raia katika jimbo la kaskazini-magharibi la Niger.

View Comments