Katika uamuzi wa kihistoria kwa wanaharakati wa haki za watu wa mapenzi ya jinsi moja, sheria zinazopiga marufuku mapenzi ya jinsia moja kati ya wanaume zimeelezwa kuwa ni kinyume cha katiba nchini Namibia.
Hukumu kwa makosa ya enzi ya ukoloni ya "ulawiti" na "makosa yasiyo ya asili ya ngono" zilikuwa nadra lakini zilichochea ubaguzi dhidi ya wapenzi wa jinsi moja ambao waliishi kwa hofu ya kukamatwa.
Hakuna sheria zilizopo zinazokataza ngono kati ya wanawake nchini Namibia.
Ndoa za watu wa jinsia moja bado ni haramu katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Baada ya hukumu ya Ijumaa kusomwa katika mahakama kuu katika mji mkuu, Windhoek, wanaharakati wa kundi la LGBTQ la Equal Namibia walichapisha picha za watu wakiwa wamekumbatiana mahakamani.
Kesi hiyo mahakamani ililetwa na mwanaharakati wa Namibia anayeitwa Friedel Dausab, kwa kuungwa mkono na shirika la misaada la Uingereza la Human Dignity Trust.
"Haitakuwa kosa tena kupenda," Bw Dausab alisema akitoa maoni kuhusu hukumu hiyo, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa "alikuwa na furaha tu".
Umoja wa Mataifa pia umepongeza uamuzi huo, na kuuita "hatua yenye nguvu" kuelekea taifa shirikishi zaidi ambalo pia litaboresha upatikanaji wa huduma za afya na matibabu ya VVU.
Kwa kuhofia kurudishwa nyuma kwa uamuzi huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linaitaka serikali ya Namibia kuhakikisha usalama na utu wa watu wa LGBTQ.