In Summary

•Kufuatia mapinduzi, nchi za Afrika Magharibi ziliwawekea vikwazo wanajeshi hao, zikilenga kuwasukuma kurejesha utawala wa kiraia haraka.

Image: BBC

Nchi tatu za Afrika Magharibi zinazoongozwa na tawala za kijeshi zitazindua pasipoti mpya za kibayometriki "katika siku zijazo" kama sehemu ya kujiondoa kutoka kwa umoja wa kikanda wa Ecowas.

Mali, Burkina Faso na Niger, ambazo viongozi wake wa kijeshi walichukua madaraka katika mfululizo wa mapinduzi kati ya 2020 na 2023, walitangaza mpango wao wa kuondoka kwenye umoja huo mnamo Januari.

Kufuatia mapinduzi hayo, nchi za Afrika Magharibi ziliwawekea vikwazo wanajeshi hao, zikilenga kuwasukuma kurejesha utawala wa kiraia haraka.

Lakini mataifa matatu ambayo sasa yanaunda Muungano wa Nchi za Sahel hadi sasa yamepinga wito huo, yakiamua kuimarisha muungano wao.

"Katika siku zijazo, pasipoti mpya ya kibayometriki ya [muungano] itasambazwa kwa lengo la kuunganisha hati za kusafiria katika eneo letu la pamoja," kiongozi wa serikali ya Mali Kanali Assimi Goïta alisema katika hotuba yake ya televisheni siku ya Jumapili.

Kanali Goïta, ambaye ni kaimu rais wa muungano wa Sahel, alizungumza siku moja kabla ya serikali za kijeshi kuadhimisha mwaka wa kwanza tangu wafanye uamuzi wa kuunda muungano wao wenyewe.

Alisema pia walikuwa wakipanga kuzindua huduma ya pamoja ambayo itakuza "usambazaji wa habari kwa usawa katika mataifa yetu matatu".

Burkina Faso ilikuwa imefichua mapema uamuzi wake wa kuzindua pasipoti mpya ya kibayometriki bila nembo ya Ecowas.

Bado haijulikani jinsi pasi hizo mpya za kusafiria zitaathiri usafiri wa raia wao kwenda mataifa mengine ya Ecowas ambako walifurahia kusafiri bila visa kama wamiliki wa pasipoti ya kikanda ya mataifa 15.

Mnamo Julai, wakuu wa serikali walisema walikuwa 'wameshaamua' kuhusu uamuzi wao huku wakiipa kisogo Ecowas.

Walisema wanataka kujenga jumuiya ya watu huru kwa kuzingatia maadili ya Kiafrika na "mbali na udhibiti wa mataifa ya kigeni".

Tangazo la hivi punde linakuja wakati Ecowas inajishughulisha na juhudi za kuyafanya mataifa matatu ya Sahel kurejea katika umoja huo.

Ecowas hivi majuzi ilionya kuwa kurasimishwa kwa kundi lililojitenga kulileta hatari ya kusambaratika kwa eneo hilo na kuzidisha ukosefu wa usalama.

View Comments