In Summary

•Hakimu Mkuu Mwandamizi Eunice Nyutu alimhukumu katika nafasi yake ya mhariri na nafasi yake binafsi.

•Hakimu alibainisha kuwa hadithi hiyo iliyochapishwa na TUKO ilikuwa imeharibu sifa ya shahidi.

Mahakama
Image: MAHAKAMA

Mhariri mkuu katika TUKO.co.ke asubuhi ya leo amehukumiwa kifungo cha miezi 6 gerezani au kulipa faini ya Sh50,000 kwa makala ya kupotosha iliyochapishwa kuhusiana na kesi inayoendelea ya NYS.

Hakimu Mkuu Mwandamizi Eunice Nyutu alimhukumu katika nafasi yake ya mhariri na nafasi yake binafsi.

Katika uamuzi wake, Nyutu alisema adhabu hiyo itakuwa funzo kwa wanahabari wengine, wahariri na vyombo vya habari dhidi ya kuchapisha makala za kupotosha.

Alibainisha kuwa hadithi hiyo iliyochapishwa na TUKO ilikuwa imeharibu sifa ya shahidi.

Katika kesi hiyo, mahakama imewaita wahariri wakuu wa TUKO na KBC kwa kuandika hadithi ya kupotosha kuhusu shahidi wa upande wa mashtaka ambaye alikuwa akihojiwa na upande wa utetezi.

Hii ni baada ya upande wa mashtaka kuibua malalamishi wakisema makala hayo yamechafua jina la shahidi wao.

Kupitia kwa wakili wake, mhariri huyo wa TUKO aliomba msamaha kwa mahakama kuhusu kisa hicho, akisema mmoja wa wanahabari wao alikuwa amewapa kisa hicho na walipogundua kosa waliondoa makala hayo.

Hata hivyo, mahakama ilisema kuandika makala ya kashfa kunaadhibiwa na sheria.

Pia ameiagiza TUKO kuchapisha ombi la msamaha kwa shahidi kwenye tovuti yao na pia kubatilisha makala ya awali iliyochapishwa.

Mahakama ilitoa wito zaidi kwa Mhariri Mtendaji wa KBC. Hakimu alikataa kusikiliza mhariri mkuu ambaye alikuwa ametumwa kumwakilisha bosi wake, akisema anahitaji mhariri mkuu.

View Comments