In Summary

•Msichana huyo alikuwa amezuiliwa katika kituo hicho pamoja pamoja na mpenzi wake wa miaka 17 na walitarajiwa kufunguliwa mashtaka.

•Mahakama ilimnyima afisa huyo wa polisi nafasi ya kuachiliwa kwa dhamana na badala yake ilimzuilia hadi Jumatano.

Pingu
Image: Radio Jambo

Afisa wa polisi anayefanya kazi katika kituo cha polisi cha Sakutiek, kaunti ya Narok amefikishwa katika mahakama ya Narok kwa madai ya kumnajisi msichana wa miaka 16 ambaye alikuwa anazuiliwa na polisi.

Anthony Leteipa Nanyukie alidaiwa kumchukua msichana huyo kutoka katika seli ya polisi hadi nyumbani kwake ndani ya kituo cha polisi ambako alilala usiku kucha Desemba 5, 2022.

Msichana huyo alikuwa amezuiliwa katika kituo hicho pamoja pamoja na mpenzi wake wa miaka 17 na walitarajiwa kufunguliwa mashtaka.

Afisa huyo wa polisi ambaye alifika mbele ya Hakimu Mkuu wa Narok Samuel Mungai alikana mashtaka hayo.

Kupitia kwa wakili wake Charles Langat, mshtakiwa aliiomba mahakama kumwachilia kwa dhamana akisema ndiye pekee anayelea watoto wake saba. Langat pia aliomba mteja wake azuiliwe katika kituo cha Polisi cha Sakutiek.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga maombi hayo ukisema afisa huyo alitenda kosa hilo katika kituo cha polisi kwa hivyo hapaswi kuruhusiwa kurudi pale kwani angevuruga ushahidi kwa urahisi.

Mahakama ilimnyima afisa huyo wa polisi nafasi ya kuachiliwa kwa dhamana na badala yake ilimzuilia hadi Jumatano ambapo hatima yake ya iwapo ataachiliwa kwa bondi itaamuliwa.

Wakati uo huo, mahakama iliarifiwa kuwa mtoto huyo alikuwa bado akipokea dawa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok huku mpenziwe mwenye umri wa miaka 17 akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

View Comments