In Summary

• Mwanamume mwingine aliyekuwa anamsambazia mafuta hayo alifungwa miaka 10 jela au kulipa faini ya milioni 10.

Afungwa miaka kadhaa jela kwa kupika chipsi kwa mafuta ya transfoma
Image: Maktaba

Elijah Mwangi Muthongo, mfanyibiashara wa vibanzi katika kaunti ya Nyandarua amepatikana na hatia ya kupika chakula hicho pendwa kwa kutumia mafuta ya transfoma baada ya kushtakiwa.

Muthongo ambaye alikuwa anafanya biashara ya kuuza chips katika mgahawa wake mdogo katika soko la Ol Kalou kaunti ya Nyandarua alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya shilingi laki mbili.

Matatizo ya Muthongo yaianza pale aliponaswa na lita kumi na moja za mafuta kutoka kwa transfoma ya umeme, alikamatwa na maafisa kutoka shirika la kusambaza umeme nchini Kenya.

"Mafuta hayo yalitumika kupika chipsi kwenye hoteli yake na pia kuuzwa kama mafuta ya kupikia ya popcorn," taarifa hiyo ilisema kwa sehemu.

Mshtakiwa mwenzake aliyetambuliwa kama Bw Zachary Mwangi Gitau, ambaye alipata kutoka kwake mafuta ya transfoma, alihukumiwa kifungo cha miaka 10 au faini ya Shilingi milioni 10 kwa kuharibu transfoma hiyo.

"Uamuzi huu ni msukumo mkubwa kwa juhudi za Kampuni kupambana na uharibifu wa transfoma kwani adhabu kali na vifungo vya jela vitazuia waharibifu," alisema Meja jenerali mstaafu Paul Nyaga, bosi wa huduma za usalama wa Kenya Power.

View Comments