In Summary
  • Kulingana na hati ya mashtaka washtakiwa hao wanasemekana kutenda kosa hilo Mei 2 kando ya Barabara ya Ngong na Langata mtawalia.
Basi la abiria lililochomwa Ngong Road wakati wa maandamano.
Image: Maktaba

Vijana kadhaa waliodaiwa kuchoma basi kando ya Barabara ya Ngong na lori huko Langata walishtakiwa katika mahakama ya Kibera Alhamisi.

Vijana hao pia walishtakiwa kwa kushiriki katika mkusanyiko usio halali kinyume na sheria.

Brian Otieno, James Otieno, Erick Tom Ochieng, Francis Maina Muriuki, James Nyamwanda, Abiud Shikukuli, Fredrick Otieno Ogada, na wengine walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mkuu Monica Maroro.

Hata hivyo walikanusha mashtaka.

Kulingana na hati ya mashtaka washtakiwa hao wanasemekana kutenda kosa hilo Mei 2 kando ya Barabara ya Ngong na Langata mtawalia.

 

Bei ya takriban ya magari hayo hata hivyo haikufichuliwa mahakamani.

Mmiliki wa gari lililoteketezwa la Isuzu Minibus KBV 362R kupitia wakili wake aliitaka mahakama kuachilia gari lake ambalo polisi walilishikilia kama kielelezo lakini mahakama ikashauri maombi rasmi yawasilishwe.

"Wacha nikupe muda wa kuwasilisha ombi rasmi la kuachiliwa kwa gari, hatuwezi kufanya mambo kwa kawaida," mahakama ilielekeza.

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 na dhamana mbadala ya pesa taslimu Sh 100,000.

Kesi hiyo itaendelea baadaye mwezi huu kwa maelekezo zaidi.

Katika maandamano hayo ambayo hata hivyo vinara wakuu hawakushiriki, visa mbalimbali vya uhalibifu wa mali ya watu viliripotiwa katika maeneo mengi nchini ambayo Odinga anajivunia kuwa na ufuasi mkubwa.

Jijini Nairobi, magari mawili yaliripotiwa kuchomwa moto na kundi la vijana ambao wanakisiwa kutumia fursa ya maandamano ya Azimio kutekeleza maovu yao.

Mmiliki wa gari hilo alivunja kimya chake na kusema kwamba dereva alimpigia simu akilia na yeye alikuwa katika hafla ya mazishi.

Jamaa huyo mwenye umri wa makamo alizungumza kwa uchungu akisema kwamba gari hilo lilikuwa ndio tegemo kubwa kwa familia yake na pia alikuwa bado anaendelea kulipia riba ya mkopo.

“Nilikuwa mazishi mahali, nikapigiwa simu na dereva na akaniambia kuwa amepatana na wahalifu huko Posta Ngong Road na akatolewa kwa gari akapigwa. Alikuwa Analia mimi nikamwambia wewe usijali,” mwanamume huyo alisema.

Alisema kuwa baadae aliitwa na makachero wa idara ya DCI ambao baada ya usaili wa muda walitaka kubaini umiliki wa gari hilo ambapo walimuomba hati na kumpa matumaini kuwa wataendelea na uchunguzi.

“Niliitwa na DCI waliniitisha logbook na wakasema watanipigia. Sasa mimi hilo gari ndilo lilikuwa linalea familia na sasa sijui vile nitafanya na hilo gari lilikuwa la mkopo,” mjasiriamali huyo mwenye uchungu alisema.

 

 

 

 

View Comments