In Summary
  • Walikiri mashtaka na Ali Mustafa aliiambia mahakama kwamba alihitaji kwenda nyumbani ili aweze kuwahudumia watoto wake.
Image: CLAUSE MASIKA

Wakimbizi wawili Jumanne waliambia mahakama ya Kibera kwamba walinyanyaswa na kupigwa na maafisa wa polisi wa Kenya walipokuwa kizuizini.

Wawili hao waliitaka mahakama kuwaruhusu kurejea nchini mwao.

Obura Hamza Okwri, Raia wa Uganda na Thiery Nishime, raia wa Burundi, walimweleza Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera Samson Temo kwamba hawakuwa tayari kuteseka zaidi mikononi mwa Mamlaka za Kenya.

"Polisi wamekuwa wakitupiga, tumeteseka hapa Kenya, turuhusu turudi katika nchi yetu," walisema kwa pamoja.

Wawili hao wanashtakiwa pamoja na Ali Mustafa na mkewe Sarah Abdullahi kwa kuanzisha fujo kwa namna ambayo huenda ikavuruga kuwepo kwa amani kinyume na sheria.

Hati ya mashtaka inasema washtakiwa walitenda kosa hilo mnamo Mei 22, 2023, saa 1200 katika Barabara ya General Mathenge katika Kaunti Ndogo ya Westlands ndani ya Kaunti ya Nairobi.

Mahakama ilisikia kwamba mshtakiwa alizua fujo kwa kuziba lango kuu la kuingilia na kurusha mawe moja kwa moja kwenye lango la afisi za Kituo cha Pamoja cha Huduma kwa Wakimbizi kilicho kando ya barabara hiyo.

Kulingana na mwendesha mashtaka wa mahakama Samson Ng’etich, washtakiwa ambao ni wakimbizi walitembelea maeneo hayo na kuanza kurusha mawe na kudai huduma fulani.

Walikiri mashtaka na Ali Mustafa aliiambia mahakama kwamba alihitaji kwenda nyumbani ili aweze kuwahudumia watoto wake.

Hakimu aliagiza washtakiwa wazuiliwe hadi Mei 30 kwa ajili ya ripoti ya uangalizi na ripoti ya watoto kuwasilishwa mahakamani.

 

 

 

 

 

View Comments