In Summary

•Hakimu Ellena Nderitu alibainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa dereva huyo kutoka Rwanda kutohudhuria vikao vya mahakama ikizingatiwa kuwa yeye ni raia wa kigeni.

•Pia alidokeza kuwa dereva huyo wa masafa marefu hana makazi au anwani rasmi ambapo anaweza kupatikana nchini Kenya.

Dereva Gilbert Mutuye katika mahakama ya Molo
Image: THE STAR

Dereva wa lori lililosababisha ajali mbaya iliyoua watu 52 katika eneo la Londiani, kaunti ya Kericho mwishoni mwa mwezi uliopita amenyimwa dhamana na mahakama  ya Molo.

Katika uamuzi wake mnamo Alhamisi, Julai 20, Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Molo Ellena Nderitu alibainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa dereva Gilbert Mutuye Mungu kutoka Rwanda kutohudhuria vikao vya mahakama ikizingatiwa kuwa yeye ni raia wa kigeni.

"Tangu kisa hicho kitokee mnamo Juni 30, hakuna ndugu au mwajiri aliyemtembelea katika kituo cha hospitali alikolazwa baada ya kupata majeraha mabaya," hakimu Elena Nderitu alibainisha.

Hakimu huyo pia alibainisha kuwa aina ya mashitaka hayo inafaa kuzingatiwa ikizingatiwa kuwa anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya wengi na mashitaka mengine mazito ya udereva mbaya ambayo yanavutia adhabu ya kifungo cha maisha jela na hivyo huenda akakwepa vikao vya mahakama.

Pia alidokeza kuwa dereva huyo wa masafa marefu hana makazi au anwani rasmi ambapo anaweza kupatikana nchini Kenya.

Dereva huyo ambaye alifikishwa mahakamani Julai 19 akiwa amekalia kiti cha magurudumu sasa atasalia chini ya ulinzi wa polisi akisubiri kesi hiyo isikizwe na kuamuliwa huku kikao kijacho kikipangwa mnamo Agosti 30.

Mutuye anakabiliwa na mashtaka 90 ya jinai mahakamani ikiwa ni pamoja na kuendesha gari hatari, hali iliyosababisha maisha ya watu 52 kupotezwa na uharibifu wa hadi magari 10.

Hapo awali, Mutuye alisema ajali hiyo ilitokea baada ya lori lake kupata hitilafu ya breki na hivyo kuwa vigumu kwake kulidhibiti barabarani.

View Comments