In Summary

• Kulingana na maafisa wa upelelezi, washukiwa hao walipoondoka rumande katika gereza la Meru GK, mmoja wao alirejea katika shughuli za uhalifu. 

Nyumba ya mbao walimokuwa washukiwa
Image: DCI/ TWITTER

Wanaume watatu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa genge la uhalifu huko Meru wametiwa mbaroni katika operesheni inayoendelea ya kuzima visa vya ujambazi katika eneo hilo. 

Maafisa wa upelelezi walisema washukiwa hao watatu wanasakwa kwa makosa kadhaa katika mahakama za Meru, Githongo na Nanyuki.Makosa hayo yanayodaiwa ni pamoja na mauaji, wizi, jaribio la kunajisi na kuvunja nyumba. 

Wakati polisi wakiendesha operesheni ya kuwakamata washukiwa, kiongozi wa genge hilo alifanikiwa kutoroka kupitia mwanya uliofichwa kwenye nyumba yake ya mbao. 

"Operesheni hiyo ya kistadi pia ilisababisha kupatikana kwa magari mawili yaliyotumiwa na washukiwa kuvuka kaunti hadi maeneo waliyolenga," wapelelezi walisema. 

Maafisa wa upelelezi pia walibainisha kuwa sehemu ya taarifa za ujasusi zinaonyesha kuwa washukiwa wawili kati ya waliokamatwa walikutana awali katika gereza la Meru GK wakiwa mahabusu kwa makosa ya unyang'anyi na mauaji na wamekuwa nje kwa dhamana. 

Kulingana na maafisa wa upelelezi, washukiwa hao walipoondoka rumande katika gereza la Meru GK, mmoja wao alirejea katika shughuli za uhalifu. 

"Mshukiwa ameongoza genge lake katika msururu wa wizi wa mabavu ikiwemo eneo la Turkwel Filling Station huko Tigania Magharibi usiku wa Aprili 24, 2023, ambapo wahudumu wa mafuta waliibiwa kwa mtutu wa bunduki," wapelelezi walisema. 

Maafisa wa upelelezi walisema katika tukio hilo la saa 2 asubuhi, waathiriwa walikuwa wamefungwa kamba baada ya kupigwa na mateke na watu wanane waliokuwa na bunduki mbili aina ya AK47. Kisha walitoweka na pesa taslimu Sh57,000 na kisanduku chenye pesa kisichojulikana.

View Comments