In Summary

•Katika tweet hiyo, Ndii alidai kuwa Mwangi alilipwa kutumia pesa za kampeni za Rais William Ruto ili kujiunga na mpango huo

•Mwangi alitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Ndii ambaye ni  mwenye kiti wa baraza la Rais la washauri wa kiuchumi, kwa madai ya kumharibia jina.

Mwanaharakati Boniface Mwangi amemshtaki David Ndii kwa madai ya kumharibia jina
Image: Hisani

Mwanaharakati Boniface Mwangi amemshtaki David Ndii kuhusu  matamshi aliyotoa  kwenye kurasa zake za twitter mnamo julai 16 mwaka huu kuhusiana na ufadhili wa Linda Katiba.

Katika tweet hiyo, Ndii alidai kuwa Mwangi alilipwa kutumia pesa za kampeni za Rais William Ruto ili kujiunga na mpango huo

Boniface ambaye ni mlalamishi alisema, ‘’Maneno hayo kama yalivyochapishwa kwenye ukurasa wa twitter wa mshtakiwa na ambayo bado yapo hadi wakati wa kufungua kesi hii,yalitolewa kwa umma na yaliweza kuonekana na watu wengi,ndani na nje ya nchi na yalikusudiwa kurejelea ,’’

Katika tweet hiyo, Ndii alisema:

“Wakati wa ufichuzi, Linda Katiba iliundwa na mimi na Martha kwa uungwaji mkono wa Ruto. Wakati huo Martha  alitarajiwa kuwa mgombea mwenza wa William Samoei Ruto. Alifichua kikamilifu ndiyo maana Makau Mutua alikuwa akinishambulia. Hata alimlipa Boniface kutoka pesa za kampeni za William Samoei Ruto. Wanafiki wote,”

Ndii alikuwa akijibu tweet ya mtumiaji anayeitwa @McOsedoh, iliyosoma,

“Siamini kwamba Bonny na Ndii waliwahi kuwa katika kundi liitwalo linda katiba wakipigania vikali utawala wa sheria na kuheshimiwa kwa katiba. Jinsi Ndii alijiunga na waasi wa Katiba ya Kenya ya  mwaka wa 2010 bado haiaminiki. Power Corrupt,”

Baada ya tweet hiyo kusambaa, Mwangi alitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Ndii ambaye ni  mwenye kiti wa baraza la Rais la washauri wa kiuchumi, kwa madai ya kumharibia jina.

Aidha mwanaharakati huyo alisema alijitolea wakati na raslimali zake kwa Linda katiba na hakuomba pesa kwa mtu yeyote.

Kwenye taarifa yake ya julai 17, Mwangi alisema,

“Sikulipwa chochote na yeyote ikiwa ni pamoja na William Ruto. Ikiwa Ndii yuko tayari kusimama na uwongo wake, basi tutakutana kortini na tutaona ikiwa ana ushahidi wa kuunga mkono uwongo wake ,”

 Martha Karua ambaye ametajwa kwenye mazungumzo haya ambaye pia alikua mwanachama wa kikundi cha Linda Katiba, alimkashifu Ndii kwa matamshi yake na kumtaja kuwa muongo. Katika tweet yake ya julai 16 akimjibu Ndii Martha alisema,:

“Nimesikitika kuwa umejiunga na safu ya waongo wasiopunguzwa. Katika ushirikiano wetu katika linda katiba hukuwahi kufichua ufadhili wowote kutoka  kwa William Samoei Ruto au mtu mwingine yeyote.Tulichangia gharama zetu hadi mwisho tulipopata ufadhili kutoka kwa mfadhili. Ikiwa kabisa William Ruto aliikufadhili, ni mambo yako binafsi,”

Aidha, Martha alizidi kusema,

“Sifahamu Boniface Mwangi kupokea pesa kutoka kwa William Ruto, nakumbuka wakati Boniface Mwangi alikuwa anaondoka hatukuweza kumrudishia gharama za mfukoni achilia mbali kumlipa,”

Katika madai yake, Bonface Mwangi alisema kuwa , madai ya Ndii ni ya uwongo na yalichochewa na chuki, kwa  dhamira za  kudhalilisha sifa zake kwani haukutegemea chembe zozote za ukweli. Aliongeza kusema kwamba Ndii alikosa kutumia busara ya kupata maoni kutoka kwake au kumuomba radhi kwa matamshi yake licha ya kutakiwa kufanya hivyo.

Aidha mahakama ya  Nairobi imempa Ndii muda wa siku 15 kujibu kesi hiyo.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, “iwapo utashindwa kufika mahakamani katika muda uliotajwa hapo juu,mlalamishi anaweza kuendelea na kesi hiyo na hukumu kutolewa kama haupo,”

View Comments