In Summary

• Hakimu alibainisha kuwa madai ya mwendesha mashtaka kwamba maisha ya Ian yatakuwa hatarini kwa sababu maafisa wengine walitaka kulipiza kisasi haitoshi.

Ian Njoroge akiwa na mamake na watu wengine nje ya gereza la Viwandani Nairobi, muda mfupi baada ya kuachiliwa kutoka rumande.
Image: HISANI

Ian Njoroge mwanafunzi wa chuo kikuu anayedaiwa kumvamia afisa wa polisi katika Barabara ya Kamiti na kumnyang'anya kifaa cha mawasiliano ameachiliwa kutoka gereza la Viwandani baada ya aliyekuwa gavana Mike Sonko kuingilia kati.

Msaidizi wa Sonko, Francis Wambua alifanikisha kuachiliwa kwa Ian Njoroge kutoka rumande baada ya kusimama kama mdhamini wake.

Wiki jana, Njoroge aliachiliwa kwa Sh700,000 na mahakama.

Hakimu mkuu wa Milimani Ben Mark Ekhubi alimwachilia Njoroge kwa dhamana baada ya kutupilia mbali ombi la upande wa mashtaka kwamba asiachiliwe kwa dhamana ili kulinda usalama wake.

Akitoa uamuzi wake, hakimu alibainisha kuwa madai ya mwendesha mashtaka kwamba maisha ya Ian yatakuwa hatarini iwapo angeachiliwa kwa sababu maafisa wengine walitaka kulipiza kisasi haitoshi kumweka mshtakiwa kizuizini.

Ekhubi pia alisema shtaka la wizi wa mababvu dhidi ya Njoroge ni kinyume cha Katiba kwa  sababu kifungu cha 96 (2) cha Kanuni ya Adhabu ambacho kilitumiwa kwa kosa hilo kiliharamishwa na Mahakama Kuu.

"Madai kwamba Ian Njoroge hapaswi kuachiliwa kwa dhamana kwa sababu ana hatari ya kukimbia hayakubaliki kwa vile hayaungwi mkono na ushahidi wowote," hakimu alisema.

View Comments