In Summary

• Mshukiwa anadaiwa kutekeleza mauaji ya wanawake watano akiwemo mtoto wa miaka mitano katika maeneo kadhaa kaunti ya Nakuru.

• Kesi dhidi ya mshukiwa kwa jina Kwame itatajwa tena katika mahakama kuu ya Nakuru tarehe 15 Oktoba.

crime scene 1

Mshukiwa wa msururu wa mauaji katika kaunti ya Nakuru amekana madai ya kuhusishwa na mauaji hayo katika mahakama ya kuu ya Nakuru.

Mshukiwa huyo kwa jina Ezekiel Sakwa Mwangi maarufu kama Kwame anadaiwa kuhusika na vifo vya wanawake watano akiwemo mtoto wa miaka 5 baada ya kuwanajisi.

Kwame alikamatwa na maafisa wa DCI mwezi Agosti tarehe 18 mwezi mmoja baada ya visa vya mili ya waathiriwa kuanza kupatikana katika shamba la mahindi.

Awali, Kwame alifikishwa mbele ya mahakama ya hakimu ya Molo ambapo mahakama hiyo ilikubali kuwapa maafisa wa upulelezi wa mauaji muda siku 30 kufanya uchunguzi zaidi.

Katika mahakama kuu ya Nakuru, maafisa wa uchunguzi wamewasilisha ushahidi wa msururu wa matukio ya mauaji waliopata dhidi ya mshukiwa.

Kulingana na uchunguzi wa maafisa hao, mnamo tarehe 13Julai, mwili wa mtoto wa miaka 5 kwa jina Alice Ayuma ulipatikana katika shamba la mahindi ukiwa na majeraha ya rungu.

Unyama huo uliendelea tena na tarehe 5 Agosti mwili wa Virginia Njeri ulipatikana na majeraha sawia.

Mshukiwa anadaiwa kuendeleza na msururu wa mauaji ambapo inaaminika alihusika na mauaji ya Florence Mueni kwa kupigwa na mwili wake kufichwa kichakani katika eneo la Kalyet.

Vile vile Kwame anashtumiwa kutekeleza mauaji mengine tarehe 7 Agosti katika mtaa wa Baraka alipomvamia Vellah Moraa na kumjeruhi.

Mahakama kuu ya Nakuru imemnyima dhamana baada ya afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ODPP kukana vikali ombi hilo.

Kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 15 katika mahakama hiyo.

 

View Comments