In Summary

• Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu, Kanyi Kimondo, Roselyne Aburili na Mugure Thande.

Mbunge la Kenya
Image: Handout

Ni pigo kwa wabunge wa bunge la kitaifa baada ya Mahakama Kuu siku ya Ijumaa kuamua kuwa Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo Maeneo bunge (NG-CDF) ni kinyume cha katiba.

Hata hivyo wabunge wamepewa takriban miaka miwili kumaliza miradi inayoendelea katika maeneo bunge yao kabla ya NG-CDF kukoma kabisa mnamo Juni 30, 2026.

Mahakama Kuu iliamua kwamba hazina hiyo ilikuwepo kinyume cha katiba baada ya kutoa uamuzi kuhusu masuala tisa kufuatia ombi lililowasilishwa na mwanaharakati Wanjiru Gikonyo baada ya Sheria ya zamani ya CDF kutangazwa kuwa kinyume na katiba.

Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu, Kanyi Kimondo, Roselyne Aburili na Mugure Thande.

Kuhusu iwapo Sheria ya CDF inakiuka muundo wa ugatuzi, mahakama iliamua kuwa Sheria hiyo inakiuka kanuni za ugatuzi.

Kuhusu kama Sheria ya CDF inakiuka muundo wa kimsingi, iliamua kwamba haikiuki muundo wa kimsingi.

Mahakama Kuu pia iligundua kuwa hazina hiyo ilikuwa inarejelea na kuingilia majukumu ambayo Katiba inapeana pekee kwa serikali za kaunti.

Kulingana na mahakama hazina hiyo pia inakiuka sheria ya ugavi wa mamlaka.

Kulingana na mahakama sheria haiwapi wabunge mamlaka ya kufanya miradi ya maendeleo bali wana majukumu ya uwakilishi, kuunda sheria na uangalizi pekee. Hazina ya CDF imekuwepo tangia mwaka 2003. 

View Comments