logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Polisi taabani kwa kumbaka mwanake ndani ya seli huko Siaya

Mlalamishi alikuwa amekamatwa na kuzuiliwa kwa kukosa barakoa.

image
na Radio Jambo

Makala15 June 2022 - 09:07

Muhtasari


•Konstabo Cosmas Chirchir pia atashtakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma mbele ya Mahakama ya Ukwala.

•Tukio hilo lilifanyika Aprili 12, 2021 wakati mlalamishi alikuwa amekamatwa na kuzuiliwa kwa kukosa barakoa.

Mahakama

Polisi mmoja kutoka kituo cha Sega, kaunti ya Siaya anatarajiwa mahakamani leo kujibu shtaka la ubakaji wa mahabusu.

Konstabo Cosmas Chirchir pia atashtakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma mbele ya Mahakama ya Ukwala.

Mshukiwa alikamatwa Jumanne baada ya uchunguzi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kubaini kuwa ana mashtaka ya kujibu.

Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) ilianzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho baada ya mwanamke mmoja kuwasilisha malalamishi kuwa alibakwa ndani ya seli ya kituo cha polisi cha Sega, eneo la Ukwala.

Tukio hilo lilifanyika Aprili 12, 2021 wakati mhasiriwa alikuwa amekamatwa na kuzuiliwa kwa kukosa barakoa.

"Mwanamke huyo alipoachiwa kutoka chini ya ulinzi alitoa taarifa za shambulio hilo la kinyama katika Kituo cha Polisi cha Ukwala na Mamlaka ikachukua suala hilo kwa uchunguzi," Taarifa iliyotolewa na IPOA Jumatano ilisoma.

IPOA imesema baada ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na kisa hicho walipendekeza kwa ODPP mshukiwa ashtakiwe kwa kosa la ubakaji.

"Baada ya kupitia kesi hiyo  kwa uhuru, ODPP ilikubali kuwa kuna ushahidi wa kutosha wa kuendeleza kesi mahakamani na kuagiza afisa huyo ashtakiwe kwa ubakaji na matumizi mabaya ya ofisi," Mwenyekiti wa IPOA Anne Makori alisema.

Makori alisema IPOA inachukulia makosa kama hayo kwa uzito mkubwa na kufichua kuwa wametumia fedha nyingi katika kesi za ubakaji.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved