In Summary

•Mikutano ya kisiasa ambayo William Ruto alitarajiwa kuhudhuria pia ilifutiliwa mbali katika dakika za mwisho na mara nyengine maafisa wa polisi wametumia vitoa machozi kuwatawanya walioudhuria.

Image: AFP

Wasiwasi wa kisiasa uliopo kati ya ndugu wawili waliokuwa katika chama tawala cha Jubilee umekuwa ukijitokeza tangu kufanyika kwa makubaliano ya kuleta amani nchini Kenya kupitia Handshake.

Tangu mwezi maamkuzi ya mkono kati ya rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake Raila Odinga yaliolenga kuleta amani nchini mnamo mwezi Machi 2018, naibu William Rito ameonekana kama mtu aliyetengwa katika maamuzi muhimu ya serikali huku vyanzo vilivyo karibu na wawili hao vikisema kwamba Ruto amefadhaishwa na serikali.

Kutengwa kwa William Ruto na wandani wake

Kuna madai kwamba naibu wa rais Wlliam Ruto alinyimwa kuingia katika makaazi yake rasmi mjini Mombasa kwa madai kwamba nyumba hiyo ilikuwa ikifanyiwa ukarabati.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti ya BBI katika ukumbi wa Bomas of Kenya Novemba 2019, William Ruto, alizuiliwa katika mkutano kati ya rais Uhuru Kenyatta na Raila , pia ilidaiwa kwamba masafara wa magari ya Ruto ulitakiwa kuondoka katika eneo hilo, baada ya Uhuru na Raila kuondoka.

Hivi majuzi naibu wa rais alizuiliwa kusafiri kwenda Uganda akiandamana na muwekezaji mmoja wa Uturuki, ambaye serikali inadai ni mfadhili wa Ugaidi.

Mikutano ya kisiasa ambayo William Ruto alitarajiwa kuhudhuria pia ilifutiliwa mbali katika dakika za mwisho na mara nyengine maafisa wa polisi wametumia vitoa machozi kuwatawanya walioudhuria.

Wakati wa sherehe za siku ya madaraka iliofanyika mjini Kisumu , Rais alivunja itikafi ambayo imekuwepo kwa kumualika Raila Odinga na wazungumzaji wengine kuzungumza baada ya naibu wa rais kumualika rais kuzungumza na taifa.

Wandani wa naibu wa rais pia hawajaepuka hasira ya rais , huku aliyekuwa waziri wa kilimo Mwangi kiunjuri na Rashid Echesa wakifutwa kazi za uwaziri. katika uongozi wa bunge , rais aliwaondoa viongozi wote wanaomuunga mkono naibu wa rais , akiwemo kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa na lile la seneti , viranja wa wengi katika mabunge yote hayo mbali na wanachama wa kamati tofauti bungeni.

Kabla ya uchaguzi wa 2013 viongozi hawa walifanya kampeni za pamoja na kuibuka washindi
Image: AFP

Katika kiwango cha chama cha Jubilee , wandani wa naibu William Ruto wameadhibiwa kupitia mfumo wa adhabu huku wabunge walioteuliwa kupitia chama hicho wakionywa kufuata maadili ya chama la sivyo waondoke.

Mikutano ya kisiasa kama ile ya chaguzi ndogo za maeneo bunge ya Kiambaa na Juja ambayo chama cha Jubilee kilipoteza kwa chama cha naibu wa rais Wiliam Ruto UDA hakujatuliza mgogoro unaondelea kati ya rais Uhuru Kenyatta na naibu wake.

Maeneo hayo ya ubunge yapo katika kaunti ya Kiambu nyumbani kwa rais Kenyatta. Kihistoria hiyo sio mara ya kwanza ambapo naibu wa rais amefadhaishwa na kunyanyaswa .

Mzozo uliotokea kati ya Jomo Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga

Tangu taifa la Kenya lilipojipatia Uhuru , Kenya imewahi kuwa na makamu wa rais 10 na naibu wa rais mmoja. Tofauti hiyo ni muhimu kwa kuwa makamu wa rais alikuwa akichaguliwa na rais na kuhudumu chini ya matakwa ya rais , hatahivyo baada ya kupatikana kwa katiba mpya ya 2010 , uchaguzi na kuapishwa kwa naibu wa rais uliwekwa katika kifungu cha 148 cha sheria kikisema kwamba naibu wa rais atachaguliwa pamoja na rais.

Hali hiyo inampatia naibu wa rais usalama wa kuhudumu ambao makamu wa rais waliopita hawakuwa nao. Mwezi Disemba 1964, wakati Kenya ilipojipatia uhuru wake , Mzee jaramogi Oginga Odinga alihusika katika kampeni ya kupigania kuwachiliwa kwa mzee Jomo Kenyatta kutoka jela na kupatikana kwa uhuru wa Kenya.

Jaramogi alihudumu kama makamu wa rais kutoka 1964-1966. Mwaka 1966, makamu wa rais Jaramogi Oginga Odinga alijiuzulu baada ya kutengwa na Rais Jomo Kenyatta.

Katika barua yake ya kujiuzulu ya tarehe 14 mwezi Aprili 1966, Mzee Jaramogi alisema kwamba Mzee Jomo Kenyatta alikataa kumtambua kuwa makamu wake katika masuala ya serikali kama sababu kuu.

''Haujanitambua mimi kama makamu wako katika masuala ya kiserikali. Ninatambua kilicho sawa kwangu na makosa, na hali hiyo inaniumiza wakati ninapokula fedha za umma bila kuwa na kazi ya kufanya. Nachukulia hili kama uharibifu wa fedha za umma na nina wasiwasi huenda kizazi kijacho kikaniuliza kuhusu uaminifu na uwazi wangu wakati watakapogundua kwamba nilishikilia wadhfa bila kazi yoyote wakati ambapo kulikuwa na umasikini katika taifa letu''.

Ushirikiano wa wawili hawa uliwashangaza mahasimu wao
Image: Getty Images

Ushirikiano wa wawili hawa uliwashangaza mahasimu wao

Baada ya kuandika barua hiyo pia alistaafu katika chama cha KANU. Alianzisha chama cha upinzani kilichojulikana kama Kenya Peoples Union KPU ambacho kilipigwa marufuku 1969 baada ya vurugu zilizotokea Kisumu , wakati Rais Kenyatta alipozuru eneo hilo ili kufungua Hospitali ya Mkoa ya New Nyanza .

Odinga aliwekwa katika kifungo cha nyumbani na baada ya kuzuiliwa na viongozi wengine wa chama chake cha KPU. Aliwachiliwa mwaka uliofuta. Katika miaka iliofuata Odinga alijaribu kujihusisha kisiasa lakini hakuweza kwasababu uhusiano wao na rais Kenyata ulikuwa umeharibika kwa kiasi kikubwa.

Wakati alipokuwa nje ya serikali. Uwezo wa Jaramogi kuandaa mipango ya kisiasa ilivunjwa , baada ya Rais Jomo Kenyatta kudhibiti eneo lake. Wandani wa Jaramogi walikamatwa au kupoteza uchaguzi kwa chama tawala cha KANU .

Mzoo huo kati ya Jomo Kenyatta na makamu wake ulianzisha uhusiano wa chuki kati ya wawili hao. Wakati wa utawala wa rais Moi , afisi ya makamu wa rais ilipunguzwa nguvu na kuwa kama ile ya msichana anayebeba maua, kwa kiongozi anayeshikilia kuonekana tu lakini sio kusikika.

Image: CHIP HIRES/GETTY IMAGES

Aliyekuwa rais Daniel Moi wakati mmoja aliuliza kandokando ya barabara mjini Limuru iwapo wadhfa wa makamu wa rais utaongeza sufuria zaidi za kupikia ugali kwa wale waliokuwa wanapigania kiongozi huyo ateuliwe.

Wakati huo afisi ya makamu wa rais iliokuwa ikishikiliwa na marehemu profesa George Saitoti ilikuwa wazi kwa miezi 18 baada ya uchaguzi mkuu wa 1997. Uwezo wote ulikuwa katika wadhfa wa urais , wakati huo wadhfa wa makamu wa rais ulipatiwa jukumu la waziri wa masuala ya ndani kama njia ya kuwafanya kuwa na kazi ya kufanya. Tukielekea katika uchaguzi mkuu wa 2002, rais Moi alimfuta makamu wa rais Profesa George Saitoti ikiwa imesalia miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi na kumchagua Musalia Mudavadi kuwa naibu wake , ambaye anashikilia rekodi ya kushikilia wadhfa wa makamu wa rais kwa muda mfuzi zaidi nchini Kenya.

Jinsi wadhfa wa naibu rais ulivyolindwa katika katiba mpya

Wakati wa kuidhinishwa kwa katiba mpya 2010, Wakenya walikasirishwa na jinsi wadhfa wa makamu wa rais ulisimamiwa , na kuamua kuchukua mtindo wa urais wa Marekani, ambapo rais na makamu wake walikuwa kitu kimoja ambapo wote watashiriki katika uchaguzi huku mgombea mwenza wa urais akichukua wadhfa wa naibu wa rais .

Katiba mpya chini ya kifungu cha 150 , pia ilitoa sababu ambazo zinaweza kumuondoa naibu wa rais katika wadhfa wake ambazo sio tofauti na zile za kumuondoa rais.

'Handshake'

Na tangu kutolewa kwa uamuzi wa mahakama ya rufaa kuhusu mradi wa BBI ulioanzishwa na rais Uhuru Kenyatta na ndugu yake Raila Odinga, uhasama kati ya rais na naibu wake umeongezeka na kufikia kiwango ambacho hakijawahi kuonekana awali.

Katika mahojiano na wahariri wakuu wa vyombo vya habari , ambao ulifanyika katika Ikulu ya rais, rais alisema wazi kwamba iwapo mtu hataki kuunga mkono mipango yake kwa mfano BBI na sera za serikali yake basi kitu ambacho angehitajika kufanya ni kuondoka katika serikali.

Bila kutaja majina , ni wazi kwamba rais alikuwa akizungumza kuhusu naibu wake William Ruto . Upande mwengine rais Uhuru Kenyatta amefanikiwa kupunguza uwezo na majukumu ya afisi ya naibu wa rais.

Naibu wa rais amebadilishwa na kuwa shabiki katika serikali alioisadia kuifanyia kampeni na kuchukua utawala. Mzozo wa kisiasa kati ya rais na naibu wake kwa kiwango kikubwa unatokana na siasa za urithi . Mapenzi ya rais Kenyatta ni kuliwacha taifa likiwa thabiti na lenye umoja chini ya kiongozi anayemuamini , huku naibu wa rais akihisi kunyanyaswa na anaamini kwamba rais anashirikiana na aliyekuwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga ili kumzuia kupata fursa ya kuwania urais.

Mzozo kati ya viongozi hao wawili umeathiri utendaji kazi wa afisi ya wafanyakazi wa umma , idara ambayo ni sharti isiwe na upendeleo wowote ili kuwapatia huduma Wakenya wote.

Wakati mwingi , wakihofia kuonekana kama wafuasi wa naibu wa rais William Ruto , maafisa wakuu wa idara hiyo wamejitenga na mikutano ya naibu huyo licha ya kwamba uwepo wao unahitajika.

Vita dhidi ya ufisadi ambavyo vimekuwa vikiwalenga wafuasi wa Ruto hivyobasi vimeonekana kukosa maadili na uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya wengi.

Sakata ambayo iliwashangaza wengi ni ile ya Covid millionaire , ambayo rais alitoa makataa ya siku 21 kufanyiwa uchunguzi kwa lengo la kuwakamata wahusika lakini hadi leo , hakuna ripoti iliowekwa wazi wala mshukiwa kukamatwa na kushtakiwa.

Hali hiyo imeweka kovu la uwazi katika vita dhidi ya ufisadi na kuchochea mtazamo kwamba vita dhidi ya ufisadi ni vita dhidi ya naibu wa rais William Ruto na wandani wake na kwamba vinashinikizwa na afisi ya juu zaidi nchini Kenya.

Uzoefu wa kidemokrasia nchini Kenya kupitia katiba mpya una miaka 11 pekee , na kwa wengi thamani ya mzozo wa kisiasa kati ya viongozi hao wawili unalenga kujaribu uwezo wake na Uhuru wake kwa taasisi huru .

Huku rais Uhuru Kenyatta akitaka kuongoza kama ilivyokuwa katika enzi za utawala wa Moi na Jomo Kenyatta wakati ambapo taasisi zote za serikali zilikuwa chini yao , uongozi huo hauwezi kuruhusiwa katika katiba mpya.

View Comments