In Summary

•Chifu wa zamani wa eneo la Kimoso, Joseph Malatit Chebii 61, alitumia siku kumi kutembea ili kuchanga fedha za kuendeleza ujenzi wa uwanja wa Kabarnet ambao umekwama kwa sasa.

•Chebii amesema kuwa hakukabiliana na watu wabaya njiani ambao walimpa maji na pesa kidogo kidogo za matumizi akiwa safarini.

•Kwa sasa anatumai kukutana na rais Uhuru Kenyatta, Mkurugenzi mtendaji wa Safaricom Peter Ndegwa na mwenyekiti wa kamati ya Olimpiki nchini Paul Tergat.

Chifu wa zamani Joseph Malatit Chebii, 61, akiwa safarini
Image: JOSEPH KANGOGO

Chifu wa zamani katika kaunti  ya Baringo alipoteza kilo tatu na jozi tatu za viatu vyake zikaharibika akiwa kwenye matembezi ya kujitolea ya kilomita 354 kufika jijini Nairobi.

Chifu wa zamani wa eneo la Kimoso, Joseph Malatit Chebii 61, alitumia siku kumi kutembea ili kuchanga fedha za kuendeleza ujenzi wa uwanja wa Kabarnet ambao umekwama kwa sasa. Aliwasili jijini Nairobi siku ya  Jumatatu.

"Nilikuwa na kilo 76 kabla ya kuanza matembezi. Nilipoteza kilo tatu katika safari yangu ya miguu kutoka Baringo" Malatit alisema.

Chebii amesema kuwa kiamsha kinywa chake cha kila siku kilikuwa chai kwa chapati na angekunywa lita nne za maji yaliyochanganywa na asali mchana.

Amesema kuwa jozi mbili za viatu vyake ziliharibika kwenye barabara mbaya na yenye milima ya kutoka Baringo kuelekea Nakuru. Jozi ya tatu iliharibikia kwenye barabara ya kutoka Nakuru kufika Nairobi.

Wanyama pori

Chebii amesema kuwa  siku ya Alhamisi alipita msitu wa kilomita 21 ulio kati ya Gilgil na Naivasha ambao una wanyamapori.

Amesema kwamba kikosi cha nyani watundu kilimfuata ila kwa bahati nzuri hakukabiliana na wanyama hatari kama simba, fisi na duma.

Ameshukuru maafisa wa trafiki ambao walimshangilia, kumtia moyo na kumhakikishia usalama wake alipokuwa safarini.

Chifu wa zamani Joseph Malatit Chebii, 61, akiwa safarini
Image: JOSEPH KANGOGO

Chebii amesema kuwa hakukabiliana na watu wabaya njiani ambao walimpa maji na pesa kidogo kidogo za matumizi akiwa safarini.

Kwa sasa anatumai kukutana na rais Uhuru Kenyatta, Mkurugenzi mtendaji wa Safaricom Peter Ndegwa na mwenyekiti wa kamati ya Olimpiki nchini Paul Tergat.

"Ujumbe wangu kwao ni wasaidie na fedha za kukamilisha ujenzi na uandalii wa uwanja wa Kabarnet. Moyo wangu utatulia tu hayo yakitimia" Alisema Chebii.

Akiwa katika matembezi yake alibeba bango lililoandikwa 'Kabarnet Stadium Tuokoe'

Siku ya Jumamosi waziri wa kazi Simon Chelugui ambaye anatoka kaunti ya Baringo aliomba viongozi na Wakenya kuunga mkono kampeni ya Chebii.

(Utafsiri: Samuel Maina)

View Comments