In Summary

•Wazazi na waalimu wengi wamejitokeza haswa mitandaoni kutoa malalamiko yao kuhusiana na mfumo huo ambao ulizinduliwa nchini mwaka wa 2017  baada ya kutupiliwa kwa mfumo wa hapo awali wa 8-4-4

•Wazazi wengi wamekuwa wakilalamika gharama kubwa ya kutekeleza mfumo huo huku wakiagiza serikali kurejesha mfumo wa zamani wa 8-4-4 ambao haukuwagharimu pesa nying

•Hata hivyo waziri wa Elimu George Magoha amesisitiza kuwa utaendelea na serikali haina nia ya kuutupilia mbali.

CBC
Image: HISANI

Hivi karibuni mfumo wa elimu wa CBC umekabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wazazi na washika dau wa elimu nchini.

Wazazi na waalimu wengi wamejitokeza haswa mitandaoni kutoa malalamiko yao kuhusiana na mfumo huo ambao ulizinduliwa nchini mwaka wa 2017  baada ya kutupiliwa kwa mfumo wa hapo awali wa 8-4-4.

Kufuatia malalamishi hayo, tayari rais wa mawakili nchini Nelson Havi ametangaza kuwa atawasilisha kesi kortini wiki ijayo akipinga mfumo huo ambao haujapokewa vizuri na asilimia kubwa ya Wakenya.

"Nimeskia kilio cha wazazi, walezi na walimu. Kesi ya kupinga CBC itawasilishwa kortini wiki ijayo. Mfumo wa elimu nchini haufai kuwa jaribio ghali, lisiofaa na ambalo halifanyi kazi kwa viongozi wetu wa kesho" Havi aliandika kwenye mtandao wa Twitter mapema wiki hii.

Wazazi wengi wamekuwa wakilalamika gharama kubwa ya kutekeleza mfumo huo huku wakiagiza serikali kurejesha mfumo wa zamani wa 8-4-4 ambao haukuwagharimu pesa nyingi.

CBC inawahitaji watoto wao kutumia vifaa vya kiteknolojia kama vile simu, kompyuta na televisheni ambavyo wazazi wamelazimika kuwatafutia watoto wao.

Baadhi ya vifaa hivyo hutumia data ama Wi-Fi ili kufanya kazi, jambo ambalo limewachokesha wazazi wengi ambao wameeleza malalamiko yao kufuatia gharama kubwa ya data na WiFi nchini.

Kando na hayo, baadhi ya wazazi wameeleza kuwa wameagizwa kuwanunulia watoto wao vitabu zaidi, hatua ambayo wengi wamehisi imewaacha na mzigo mkubwa mgongoni.

Sio vitabu pekee kwani mfumo wa CBC unawahitaji watoto kujua kufanya kazi za kinyumbani kama vile kupika, kuosha, kushona n'k. Kufuatia hayo wazazi wanahitajika kunulia watoto wao vitu vinavyohitajika kufanya mafunzo hayo kama vile vyakula na vifaa vya kushona.

Isitoshe, wazazi wengine wamelalamika kuwa wamelazimika kusaidia watoto wao kufanya nyingi kazi za ziada ambazo wamekuwa wakipewa shuleni.

Kwenye mfumo wa CBC wanafunzi wanahitajika kujua namna ya kutengeneza vitu kama vile 'scarecrow', magari ya kuchezea, vifagio miongoni mwa vitu vingine. 

Baadhi ya wazazi wanahisi kuwa kazi zile zinachokesha haswa kuona kuwa wanalazimika kuzifanya pamoja na watoto wao mida ya jioni wakati kila mmoja amerejea nyumbani.

Hali hii imewafanya wazazi kutia msukumo kwa serikali itupilie mbali mfumo wa CBC ambao sasa uko katika mwaka wake wa tano.

Hata hivyo waziri wa Elimu George Magoha amesisitiza kuwa utaendelea na serikali haina nia ya kuutupilia mbali. 
View Comments