Image: BBC

Kwa sababu ya ustawi wa teknolojia kuna taaluma ambazo zinatokomnea na iwapo ulipanga kuzifanya ama unazifanya kwa sasa, basi wakati umewadia kuanza kufikiria kuhusu kingine unachoweza kufanya ili kujikimu kimaisha.

Fahamu baadhi ya taaluma ambazo zinapotea kabisa katika miaka michache ijazo.

Dereva

Je! Wewe ni dereva wa lori, basi au chombo kingine cha usafiri na una wasiwasi juu ya kupoteza kazi yako?

Kulingana na dunia jinsi inavyokwenda, bila shaka ni haki yako kuwa na wasiwasi

Hii ni kwa sababu mapinduzi katika sekta ya usafirishaji yanaendelea ambayo yatabadilisha sekta hiyo yote.

Kuna mamilioni ya watu wanaopata kipato chao kupitia kazi ya udereva hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa mamilioni ya wafanyikazi wakapoteza ajira.

Madereva wa teksi, madereva wa basi, madereva wa malori, madereva wa uber na madereva wa uwasilishaji bidhaa na wengineo wana hofu kutokana na mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza taratibu.

Kulingana na utafiti wa Goldman Sachs, inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 3 nchini Marekani watapoteza kazi zao kwa sababu ya kuhamia kwenye teknolojia ya usafiri wa kujiendesha wenyewe.

Kutokana na hilo, kadiri teknolojia itakavyokuwa inaendelea kubadilika na kujiimarisha, mabadiliko yatakuwa yanaendelea kutokea tena kwa kasi. Na pengine ndani ya kipindi cha miaka 25 ijayo na kuendelea, watakaokuwa wamesalia kama madereva watakuwa ni kidogo sana.

Teknolojia imeendelea kuchukua nafasi ya utamaduni uliozoeleka: wafanyikazi wasio na shahada ya chuo kikuu, au ambao wana kiwango cha chini cha elimu wameweza kupata maisha mazuri katika sekta ya uchukuzi.

Lakini sasa kazi hizo zitatoweka milele huku kazi zenye kujumuisha "Teknolojia ya habari" zikiwa na soko kubwa.

Daktari

Hii inaleta utata kidogo kwa sababu watu wengi wanataka kutunzwa au kutibiwa na mtu wanaye muona.

Janga la corona limekaribisha mabadiliko katika sekta ya afya. Imedhihirika kwamba madaktari wenyewe wanaweza kuwa na kipindi kigumu kubaini ugonjwa fulani ulitokea ghafla na hata kupata tiba yake.

Kazi hii inatishiwa kwa sababu teknolojia imeleta matumizi ya 'telemedicine' ambapo unaweza kutibiwa na daktari aliye mbali nawe kupitia njia ya video.

Hilo litahitaji kuwepo madaktari wachache tu kwani moja anaweza kuwahudumiwa watu wengi kupitia njia hizo za kisasa .

Pia imejitokeza wazi kwamba kuna uwezekano mkubwa wa watu kuamua kuingia kwenye taaluma nyinginezo kwa sababu janga la corona limedhihirisha kuwa walio mstari wa mbele katika sekta ya afya ndio walio katika hatari zaidi ya kuathirika kutokana na maambukizi.

Na hili linaweza kuchangia kupungua kwa wahudumu wa afya siku zijazo.

Nina amini kwamba tunakaribia kushuhudia mapinduzi mengine katika nyanja hii.

Hakuna daktari hata mmoja aliye na maarifa yote ya kugundua magonjwa mbali mbali na pia hawana data zote za kihistoria za mgonjwa na matibabu yanayowezekana kupatikana kwa haraka.

Mkutubi: Msimamizi wa maktaba

Inauma sana lakini siku za kufanya utafiti na kusoma katika maktaba zimepitwa na wakati.

Na sasa hivi maktaba ya kidijitali ndio iliyopo katika sehemu nyingi duniani.

Wakutubi ni walinzi wa habari za ulimwengu na maoni, mawazo, wakifanya jukumu muhimu la kidemokrasia.

Kwa upande mmoja, wakutubi wanasaidia sana, wakikuelekeza kwenye chanzo sahihi, wakitoa maoni zaidi, na kwa ujumla kusimamia mkusanyiko wa matukio kwa usahihi.

Lakini sasa hivi, huduma za maktaba za mtandaoni ndio zilizo maarufu katika vyuo vikuu na hata kwenye maeneo ambayo hilo haliwezi kuepukika watu wanageukia mtandaoni na kufanya uendelezaji wa njia ya tangu jadi ya upataji taarifa kuonekana kuwa ya gharama nyingi.

Mfano, sasa hivi vitabu vinapatikana kwenye mtandao wa Google (imekuwa biashara inayoendelea kushamiri) kiasi cha hata matumizi ya huduma hizo mitandaoni kuundiwa sheria na kufanywa kuwa imara zaidi.

Keshia yaani mtunza hela

Katika siku za kale, ilibidi kuwe na mtu wa kukagua, kuchukua pesa zako na kukupa salio kama uko nalo au kuangalia kadi yako ya mkopo.

Lakini mambo yamebadilika na sasa hivi tunasonga haraka sana kuwa na jamii isiyotumia pesa taslim.

Njia zilizoboreshwa zinazojihusisha na miamala kama vile utoaji na utumaji wa pesa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine moja kwa moja, programu kadhaa wa kadhaa za ulipiaji wa bidhaa na hata huduma ya pesa za kidijitali zinapatikana.

Tunakoenda, hivi karibuni kutakuwa hakuna haja hata ya mtu kukupa salio lako la pesa taslim kwa mkono.

Hii ni kwa sababu, kompyuta zitatimiza mahitaji yote ya kibenki tuliyo nayo.

Hata hivyo, ingawa sio kila mmoja amekumbatia njia hii huku wengine bado wakiwa wanapendelea mfumo wa pesa taslim ili kufuatilia kwa karibu matumizi yao, ukweli ni kwamba mfumo huo unaendelea kutoweka kwa kasi ya ajabu.

Katika mataifa yaliyoendelea au maeneo ya hadhi ya juu, kuna hata mashine zenye bidhaa unazoweza kuzinunua huku kukiwa na sehemu maalum ya kuweka pesa kwa ajili ya manunuzi na mashine hiyo hiyo itakutolea salia lako sahihi bila kuwepo kwa mhudumu yeyote.

Wafanyakazi wa Benki

Benki nyingi sasa hivi zinapunguza watu wanaoajiri kwa sababu shughuli nyingi za miamala zinafanywa kwa njia ya kidijitali.

Tunakoelekea ni kwamba, itafika wakati matawi mengi ya benki yatakuwa hayana budi zaidi ya kufungwa kwa sababu shughuli nyingi za benki zinafanywa kwa njia ya mtandao.

Pia kizazi cha sasa mara nyingi kinatumia njia za kidijitali katika mahitaji yake ya uwekezaji.

Aidha, benki zinashirikiana na huduma za miamala zinazotolewa na watoaji wa huduma za simu za mkononi kurahisisha mambo.

Wakati wateja wanaendelea kufurahia huduma zinazotolewa kwa njia ya dijitali, hii inamaanisha kwamba watu kidogo zaidi na zaidi watakuwa wanahitajika kama washauri wa fedha na wahudumu wa benki.

 

 

 

View Comments