In Summary

•Ingawa haijanakiliwa kwa Bibilia ama kutajwa kama mojawapo ya mila na desturi za jamii, sio wanaume wengi utakaopata wakikubali kujitosa kwenye ndoa na wanawake wenye umri mkubwa  kuwashinda.

Pete
Image: SERENDIPITY DIAMONDS

Ni dhahiri kuwa asilimia kubwa ya wanaume wanapendelea kuchumbiana na kufunga ndoa na wanawake ambao wana umri mdogo kuwashinda.

Hili ni jambo la kawaida kote ulimwenguni na ukiangazia ndoa nyingi utagundua kuwa aghalabu mwanaume huwa amempiku mkewe kwa angalau mwaka mmoja kwenda juu.

Ingawa haijanakiliwa kwa Bibilia ama kutajwa kama mojawapo ya mila na desturi za jamii, sio wanaume wengi utakaopata wakikubali kujitosa kwenye ndoa na wanawake wenye umri mkubwa  kuwashinda.

Wanaume ambao huoa wake wenye umri mkubwa mara nyingi hujipata wakikosolewa sana na hupokea upinzani mkubwa kutoka kwa jamii kufuatia maamuzi yao.

Kunazo sababu kwa nini wanaume huogopa kujiingiza kwa ndoa ambazo wao ndio wadogo kuliko wake zao;-

1. Hofu ya kusemwa na jamii

Mwanaume anaweza kupata kipenzi cha moyo wake kisha akakosa kumuoa baada ya kugundua kuwa amempiku kiumri kwa hofu ya kusemwa na jamii.

Jambo hili limewatendekea wengi ambao hushinikizwa na itikadi zilizoko katika jamii kuhusu suala la kuoa mke aliye na umri mkubwa.

Wengine huogopa kuchekwa na kutusiwa kwani hilo ni jambo la kawaida haswa hapa nchini Kenya. 

Kunao baadhi ya wanaume mashuhuri ambao wamejipata wakikosolewa sana na wanamitandao baada yao kufunga ndoa na wanawake wazee kuwaliko.

Wanajamii wengi kwa kawaida huwa  hawalichukulii jambo hilo kuwa la kawaida.

2. Heshima

Kitu kimoja ambacho hufanikisha kufaulu kwa ndoa ni heshima kati ya wapendanao.  Kunazo ndoa nyingi ambazo zimevunjika kufuatia ukosefu wa heshima.

Kuna hofu katika jamii kuwa huenda mwanamke mwenye umri mkubwa kuliko mumewe akakosa kumpa heshima kwa kuwa ameishi miaka mingi na kuona mengi kumliko.

Inaaminika kuwa akili ya mwanamke hukomaa haraka kuliko ile ya mwanamume. Kuna msemo ambao hutumika sana unaosema kuwa 'Mwanaume na mwanamke wenye umri sawa hawako sawa kimawazo"'

3. Itikadi kuwa wanawake huzeeka haraka kushinda wanaume

Jinsi wanaume huzeeka ni tofauti na wanawake wanavyozeeka. Wanawake hupata mabadiliko makubwa ya homoni zaidi ya wanaume na jambo hilo laweza  kufanya waonekane wazee kushinda wenzao wa kiume wa rika moja.

Hili ni jambo lingine ambalo hufanya baadhi ya wanaume kuhofia kujitosa kwenye ndoa na wanawake wenye umri mkubwa kuwashinda.

Wasiwasi kuwa wake zao huenda wakazeeka haraka huwashinikiza kutafuta wanawake wenye umri mdogo kuwashinda.

Inaamika kuwa wanawake wanapofikisha umri wa miaka 55 wengi wao hupoteza uwezo wa kubeba ujauzito. Huenda mwanaume akaogopa  kuoa mwanamke anayekaribia kufikisha umri huo kwa hofu kuwa hataweza kupata mtoto.

4. Tamaduni

Kunazo baadhi ya jamii barani Afrika ambazo huamini kuwa kitendo cha kuoa mke mzee kukushinda ni mwiko.

Kunazo jamii ambazo huruhusu wanaume wenye umri mkubwa kulipa mahari ya msichana mdogo na kusubiri hadi abalehe ili amuoe rasmi.

Jamii kama hizo hushikilia tamaduni kuwa mwanaume anafaa kuoa mwanamke mdogo kwani vile ndoa itaweza kustawi na kuwa na heshima.

5. Shinikizo la rika

Shinikizo la rika ni mojawapo ya mambo ambayo huathiri tabia na matendo ya kila mmoja wetu maishani.

Mara nyingi binadamu hupendelea kufuata nyayo za wenzao haswa wale ambao ni wa rika moja nao.

Mwanamume anapogundua wenzake wengi wanaandama wanadada walio na umri mdogo kuwaliko, kuna uwezekano mkubwa wake kupata shinikizo la kufanya kama wao.

View Comments