In Summary

• Walizaliwa wakiwa na jinsia moja ya kike na majina wanatumia ya kike , lakini inapofika mbele wanaanza kubadilika kijinsia.

• Mama anaeleza kuwa jinsia tata ilianza kujitokeza na ikawa yule binti wake ameanza kumea jinsia mbili ya Kike na ya kiume.

Bi.Asha* ambaye jina lake ni la kubuni , kutokana na hali ya usiri  mkuu ambao uliikumba jamii yake kuhusiana na suala linalowahusu wanae watatu ambao aliwazaa na matatizo ya kuwa na Jinsia tata(aina ya huntha) , anaonelea salama akiwa bado hajajiweka wazi kwa umma, Ila ambacho ametamani kukiweka wazi ni simulizi la kuwazaa wanawe hawa na changamoto ambayo ameishi nayo sasa kwa miaka 19 tangu alipojifungua mtoto wake wa kwanza akiwa wa kike ila baadaye baada ya Jinsia ya kiume kujitokeza ilibidi afanyiwe upasuaji ambao uliondoa jinsia ya kike na hatimaye mwanae akaanza kuishi maisha kama kijana wa kiume kama alivyoeleza mama huyu .

"Shida walio nayo hawa watoto sio kwamba wanaumwa au hawajiwezi hapana , ila afadhali ingekuwa hivyo kwani ingeeleweka , ila shida walionayo ni ya jinsia zao ziko tofauti , yaani walizaliwa wakiwa na jinsia moja ya kike na majina wanatumia ya kike , lakini inapofika mbele wanaanza kubadilika kijinsia "anasema Asha.

Mama huyu ni Mkazi wa Bukoba nchini Tanzania , akiwa na miaka 43 sasa amekuwa na mahangaiko mengi yanayohusu wanawe watatu wa kwanza waliozaliwa na changamoto za jinsia tata.

Safari yake ya uzazi ilikuwaje?

Anakumbuka aliposhika mimba ya kwanza alijawa na furaha isiyo kifani .Muda wa kujifungua ulipowadia na kumpakata mtoto wake alikuwa na muonekano wa jinsia ya kike kwa hio alipewa jina Jane*  (si jina halisi).

Aliendelea kumpa malezi kama mtoto wa kike hadi alipohitimu miaka 8 na mambo yakaanza kubadilika.

Mama huyu anaeleza kuwa jinsia tata ilianza kujitokeza na ikawa yule binti wake ameanza kumea jinsia mbili ya Kike na ya kiume . "Alizaliwa  na jinsia ya kike na tukampa majina ya kike , na mavazi yake yalikuwa ya kike , lakini kukuwa ukiangalia matendo yake muonekano wake ulianza kuegemea wa kiume .Ikawa sasa anaonekana kituko wa ajabu sana lakini sisi hatukujali baadaye akabadilika wakati jinsia ya kiume ilipojitokeza "anakumbuka Bi.Asha.

Halikuwa Jambo Rahisi kwa mama huyu kwani katika kipindi hicho hicho mabadiliko ya mwanae Jane yanajitokeza, alikuwa amejifungua  mtoto wa pili na wa tatu mtawalia na wote wakawa ni watoto wa kike na kupewa majina ya kike , kumaanisha kwamba walikuwa wamepokelewa na kulelewa kama mabinti .ila walipohitimiza miaka 13 mabadiliko kama ya mwanae wa kwanza yalianza , na hadi sasa watoto wa Bi. Asha wanaishi na jinsia mbili ya kike na ya kiume , wakiwa katika hospitali moja nchini Tanzania wakifanyiwa vipimo ili kubaini watasalia na jinsia ipi kati ya ile ya kike na kiume .

"Hawa watoto wengine ni kama tu hali ya mtoto wa kwanza kwa mfano wa pili tulianza kugundua mabadiliko kwa sauti ikawa ni kama ya kiume ,watatu naye hivyo hivyo na wote hapo walipo ni kwamba zile sehemu zote mbili zipo , wanakwenda haja zao kupitia sehemu ya kike lakini tayari za kiume zimeshaota , ila kwa sasa wanafanyiwa vipimo hospitalini  "Mama huyu anasema.

Hali hii ilibadilisha mkondo wa jamii ya Bi.Asha kutokana na kutoelewa ni vipi ajifungue watoto wake watatu wakiwa na jinsia moja ila baadaye wanakuwa na jinsia tata ? jambo ambalo limekuwa chanzo cha kumchanganya mama huyu hasa kwa kuwa jamii iliyomzunguka pia walifahamu shida hii licha ya kuwa ilisalia siri ya familia yake , ila hawakuwa na jawabu la chanzo cha hali hiyo  .

'Nilijiuliza ipi hatima yangu'?

''Kinapokuja kitu kigeni ambacho hujawahi kukiona na kukisikia inakuwa ngumu, unakuta tupo wakinamama wengi katika jamii , kila mmoja anatamani kulea mtoto wake akiwa mzima , afya njema na anayeeleweka ,kuwa ni binti au ni kijana . lakini sasa mimi inakuwa vigumu kueleza ikiwa ninazaa mtoto wa kiume au wa kike ? ninapoona wenzangu wana watoto wanaeleweka naona vigumu sana nitamuuliza Mungu maswali gani sasa ? " Bi Asha anasema

Ila alipiga moyo konde na kuendelea na maisha yake. Miaka iliyofuata baada ya kujifungua hao wanae wenye jinsia tata , alibarikiwa na watoto wengine wanne wote wakiwa hali sawa watatu wa jinsia ya kiume na mmoja wa jinsia ya kike .

Mchakato wa kutafuta usaidizi kwa wataalam ulianzishwa na mwanae wa kwanza 'Jane' akiwa na umri wa  miaka  14  .Alipoanza kuwa na ufahamu wa mabadiliko ndani ya mwili wake , aliamua kutafuta usaidizi wa kimatibabu pamoja na wafadhili ili wataalam wabaini alifaa kuishi na Jinsia ipi kati ya kike na aliyozaliwa nayo au ile ya kiume ambayo ilikuwa imeanza kumea pindi baada ya kuafikia miaka 8. Tulipata fursa ya kukutana na huyu 'Jane' ila kwa sasa anafahamika kama Tom* (si jina halisi). Jina hili alipewa baada ya jinsia ya kike kuzibwa na kuachiwa na jinsia ya kiume akiwa na miaka 17 , baada ya vipimo vya hospitalini kumuorodhesha kama mtoto wa kiume na sio wa kike tena .

"Mimi nililelewa kama binti miaka yangu ya kwanza 14 , mabadiliko mengi yalianza wakati navunja ungo nikawa na muonekano wa kiume .Cha kustaajabisha pia ni kwamba sehemu ya kiume ilianza kumea mkabala na sehemu yangu ya kike .Ulikuwa wakati mgumu na nilikuwa sijamweleza mama chochote muda mabadiliko haya yanafanyika "Tom anasema Japo Tom anasema kwamba maisha yalibadilika sana aliamua kutafuta usaidizi. Alikaa hospitalini kwa miezi huku uchunguzi ukifanywa hadi ilipoamuliwa na wataalam kwamba jeni zake zilikuwa na mfumo wa kiume na ndipo alifanyiwa upasuaji wa kurekebisha maumbile na kuachiwa na ya kiume . "Vipimo vilivyofanywa vilionesha kwamba ndio nilikuwa nimezaliwa na ishara ya mtoto wa kike ila viungo vyangu vya ndani viliashiria kuwa nilikuwa na vya kiume.Nilifanyiwa upasuaji ambao sasa uliniacha nikiwa mwanamume kamili na ndipo kukawa na mabadiliko katika majina pamoja na vyeti vyangu vyote ."anasema Tom Tom anasema kwamba tangu upasuaji huo yeye amekubali kwamba  ni mwanamume kamili , tulipomuuliza swali kuhusu hisia zake za kimapenzi zimeegemea upande upi  kuwa ameishi katika hali ya kuwa na jinsia mbili alijibu ; "Kwangu mimi hata wakati ule nilipoanza kupitia kipindi cha kubalehe kabla ya upasuaji , hisia zangu zilikuwa zimeegemea sana kama za kiume , najisikia kama anavyojisikia kama mwanamume yeyote ule kihisia "Tom anasema.

Kwa kuwa Tom ameishi kama Binti kwa  miaka 14 , anasema kwamba kuishi kwa mwili wa binti na hivi sasa kama mwanamume kuna changamoto  nyingi hasa kwa mtizamo wa kijamii."Mfano kama vile nilizaliwa , nikawa nimepewa jina ambalo ni la kike na kwa huku nyumbani nikawa hata nimetobolewa masikio nikawa hadi navaa mavazi ya kike ,kwa hiyo hatua ya kubadilika na kuwa sasa ni mwanaume ikawa ni hatua ya kustaajabisha sana hasa kwa macho ya jamii . Na hali hii ilinikosesha vitu vingi sana hasa kutokana na mchanganyiko huo nikawa hata katika shule ya sekondari nasoma na matatizo mengi sana'' Tom anasema. Asha na mwanaye Tom wana shauku kubwa ya kuhakikisha kwamba hawa ambao kwa sasa yeye anawatambua kama dada zake ila wanaishi kama huntha mmoja akiwa sasa amehitimu miaka 15 na mwingine 17 mtawalia watapata usidizi kwa wakati.

Haijawa rahisi kwa jamii hii kuishi na siri hii kubwa na kwa kujitokeza kwa umma wanasema ni katika hali ya kuelimisha jamii kwamba masuala haya yapo , na ni vyema wanaonyanyapaa watu walio na changamoto za jinsia tata wafahamu barabara yenye utelezi ambayo Tom, Kaka zake pamoja na mama yake wanapitia kila siku. "Hawa kaka zangu , kwa vile najua hali niliyopitia na sio tu kujua hata changamoto zake , binafsi yale ninayofanya mimi nikuwatia moyo sana kwasababu ya ugumu uliyopoa na ninajua kwamba wanapitia hayo hayo kwa upande wa kubaguliwa na kutengwa .Na natumai kuwa kutawadia wakati wao pia watakuwa huru baada ya wao kupata matibabu yanayofaa ilikutatua swala kuhusu jinsia yao kamili"anasema Tom Tom anasema anapenda vitu vingi kwa mfano yeye anapendelea kusoma vitabu sana , na pia amekuwa na faraja kubwa ya kucheza soka au mpira wa miguu na pia kutazama .Mwisho wa siku Tom na mama yake Asha wanamatumaini kwamba mwisho wa siku jamii itaanza kutizama watu wanaoishi na hali kama yake na ndugu zake kama watu wanaishi na ulemavu kama wa ngozi na kadhalika , Badala ya kuwatizama na unyanyapaa na kama viumbe wa ajabu . Lakini Je maoni ya wataalamu kuhusu hali hii ni ipi?

Tulimhoji Daktari Bingwa wa masuala ya kizazi Daktari Joshua Gerison akiwa Dar es Salaam ambaye anasema kwamba hali ambayo imekumba hawa watoto watatu katika jamii moja imesababishwa na hitilafu za maumbile yao au jeni .

Dkt.Gerison anasema kwamba sababu kamili ya jambo kama hili kujitokeza ni tofauti tofauti , mara nyingi anasema ni matatizo ya kimaumbile ambapo unakuta kwamba mtoto amezaliwa na vinasaba ambavyo vimezidi 46 kipimo ambacho kinatakiwa ili jinsia ya mtu itambulike vyema. "Binadamu kuzaliwa na jinsia mbili ni hali ambayo iko  kwenye jamii zetu , Binadamu kuzaliwa wakati mwingine tunafikiria ni wa kike lakini kiualisia ni wa kiume , na kinyume cha hivyo , Hii inatokana na maumbile ya nje ya muonekano wa binadamu na kuna maumbile ya ndani ambayo huwezi kuyaona lakini ukifanyiwa uchunguzi wa maabara ndio inabainisha kumbe huyu ni wa kiume au wa kike "anasema Daktari Gerison. Daktari anasema kwamba  jinsia tata zina viashiria tofauti kwa hiyo kila moja inahitaji matibabu kulingana na muonekano wa maumbile yao kwa ndani na nje  .Kwa hiyo Daktari anasema kwamba hali inayoathiri jamii ya Bi. Asha ipo na watu hawa wataweza kuishi maisha ya kawaida .  "Maisha ya kawaida anaweza akaishi lakini huenda wataathirika kisaikolojia , mtoto wa miaka 12 anakuwa amejitambua kwa jinsia aliyozaliwa nayo , sasa ghafla unataka umbadilishe jinsia , kwa mfano alikuwa wa kike sasa unambadilisha kuwa wa kiume , hapo kuna kuwa matatizo ya kuwaelewesha ili wakubali na pia jinsi ya kusonga mbele na maisha yao . "Daktari anasema.

View Comments