In Summary

•Inatokea zaidi katika sehemu za nchi za Afrika ya kati na magharibi, karibu na misitu ya kitropiki.

•Dalili za awali ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, uvimbe, maumivu ya mgongo, kuuma kwa misuli na udhaifu wa mwili kwa ujumla.

Image: BBC

Kisa kingine cha virusi vya monkeypox kimeripotiwa nchini Uingereza baada ya mtu ambaye alikuwa amesafiri hivi majuzi nchini Nigeria kugundulika kuwa na virusi hivyo nchini Uingereza. Hapa tunaangalia ugonjwa huu adimu, ambao haujulikani sana.

Monkeypox iko kiasi gani?

Monkeypox husababishwa na virusi vya monkeypox, kirusi wa familia moja ya virusi vya ndui, ingawa sio kali sana na wataalamu wanasema uwezekano wa kuambukizwa ni mdogo.

Inatokea zaidi katika sehemu za nchi za Afrika ya kati na magharibi, karibu na misitu ya kitropiki.

Kuna aina mbili kuu za virusi - Afrika Magharibi na Afrika ya Kati.

Wagonjwa wawili kati ya walioambukizwa nchini Uingereza walisafiri kutoka Nigeria, kwa hivyo kuna uwezekano kwamba wanaugua aina ya virusi vya Afrika Magharibi, ambayo kwa ujumla ni ndogo, lakini hii bado haijathibitishwa.

Kisa cha tatu kilikuwa mfanyakazi wa afya ambaye alipata virusi kutoka kwa mmoja wa wagonjwa.

Kesi nne za hivi karibuni - tatu huko London na moja kaskazini-mashariki mwa Uingereza - hazina uhusiano wowote unaojulikana, au historia yoyote ya kusafiri. Inaonekana walipata maambukizi Uingereza.

UKHSA inasema mtu yeyote aliye na wasiwasi kwamba anaweza kuambukizwa anapaswa kuona mtaalamu wa afya, lakini awasiliane na wataalamu wa afya kabla ya kufika kituo cha afya.

Dalili ni zipi?

Dalili za awali ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, uvimbe, maumivu ya mgongo, kuuma kwa misuli na udhaifu wa mwili kwa ujumla.

Mara baada ya homa, upele unaweza kutokea, mara nyingi huanza kwenye uso, kisha kuenea kwa sehemu nyingine za mwili, kwa kawaida viganja vya mikono na nyayo za miguu.

Upele, ambao unaweza kuwasha sana, hubadilika na kupita hatua tofauti kabla hatimaye kutengeneza kipele, ambacho hutumbuka baadaye. Vidonda vinaweza kusababisha makovu.

Maambukizi kawaida huisha yenyewe na hudumu kati ya siku 14 na 21.

Je, unaipataje?

Monkeypox inaweza kuambukizwa wakati mtu yuko karibu na mtu aliyeambukizwa. Virusi vinaweza kuingia mwilini kupitia ngozi iliyo na jeraha au michubuko, kwa njia ya upumuaji au kupitia macho, pua au mdomo.

Inaweza pia kuenezwa kwa kugusana na wanyama walioambukizwa kama vile nyani, panya na kindi , au kwa vitu kama vile matandiko na nguo.

Je, ni hatari kiasi gani?

Kesi nyingi za virusi ni hafifu, wakati mwingine hufanana na tetekuwanga, na huisha yenyewe ndani ya wiki chache.

Ugonjwa huu wakati fulani unaweza kuwa mkali zaidi, hata hivyo, na imeripotiwa kusababisha vifo Afrika Magharibi.

Mlipuko uko kwa kiasi gani?

Virusi hivyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza kwa tumbili aliyefungwa na tangu 1970 kumeripotiwa milipuko ya hapa na pale katika nchi 10 za Afrika.

Mwaka wa 2003 kulitokea mlipuko nchini Marekani, mara ya kwanza ugonjwa huo kuonekana nje ya Afrika. Wagonjwa walipata ugonjwa huo kutokana na kuwasiliana kwa karibu na mbwa wa mwituni ambao walikuwa wameambukizwa na aina mbalimbali za mamalia wadogo walioingizwa nchini. Jumla ya kesi 81 ziliripotiwa, lakini hakuna iliyosababisha vifo.

Mnamo 2017, Nigeria ilikumbwa na mlipuko mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa, takriban miaka 40 baada ya nchi hiyo kuwa na visa vyake vya mwisho vilivyothibitishwa vya monkeypox. Kulikuwa na kesi 172 zilizoshukiwa za monkeypox, na 75% ya waathiriwa walikuwa wanaume wenye umri wa kati ya miaka 21 na 40.

Matibabu ni nini?

Hakuna matibabu yake, lakini milipuko inaweza kudhibitiwa kwa kuzuia maambukizi.

Chanjo dhidi ya ndui imethibitishwa kuwa na ufanisi wa 85% katika kuzuia monkeypox, na bado wakati mwingine hutumiwa.

Je, umma unapaswa kuwa na wasiwasi?

Wataalamu wanasema hatari kwa umma ni ndogo.

Prof Jonathan Ball, profesa wa stadi za virusi, Chuo Kikuu cha Nottingham, alisema: "Ukweli kwamba ni mtu mmoja tu kati ya watu 50 walioambukizwa unaonesha jinsi virusi hivyo havina uwezo wa kuambukiza.

Dk Nick Phin, naibu mkurugenzi, Huduma ya Kitaifa ya Maambukizi katika Afya ya Umma Uingereza (PHE), aliongeza: "Ni muhimu kusisitiza kwamba monkeypox haisambai kwa urahisi kati ya watu na hatari ya jumla kwa umma ni ndogo sana."

PHE inafuatilia wale ambao wamekuwa na mawasiliano ya karibu na mgonjwa ili kutoa ushauri na kuwafuatilia inapobidi."

View Comments