In Summary

•Magavana wanatarajiwa kuapishwa Alhamisi tarehe 25 kwa muujibu wa sheria au katiba ndiposa waanze kazi rasmi.

•Shinikizo ni kubwa sana kutoka kwa wakenya ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi kwa ahadi za uongo huku waliowateua wakizidi kusowera.

Gavana wa kwanza wa Nairobi Evans Kidero akiapishwa Bustani ya Uhuru Park mnamo tarehe 27 mwezi machi mwaka 2007.
Image: MAKTABA

Magavana wako katika shinikizo kutimiza ahadi walizowapa raia katika msimu wa kampeni za uchaguzi mkuu uliokamilika wiki mbili zilizopita.

Katika kinya'nga'nyiro ambacho kulishuhudia wanasiasa wenye ushawishi mkuu wakibwagwa, watakaoshikilia nyadhifa hizi hawana budi ila kutekeleza wajibu wao ipasvyo bila ubaguzi na utepetevu.

Maafisa hawa wakuu watendaji wanatarajiwa kuapishwa Alhamisi tarehe 25 kwa muujibu wa sheria au katiba ndiposa waanze kazi rasmi.

Katiba mpya ya mwaka 2010, inawapa magavana mamlaka ya kufanya maamuzi kwa niaba ya gatuzi hali kadhalika kutekeleza miradi inayoambatana na matakwa ya jamii husika. Miradi hii pia inaweza kuwa ile iliyopitishwa na serikali kuu.

Kampeni za uchaguzi wa agosti 9 zilishamiri ahadi na hakikisho tele kutoka kwa magavana na wanasiasa wengine huku kila mmoja akionyesha ubabe na ujeba wake wa kuwa na suluhu ya shida zinazowakumba raia jambo ambalo liliwashawishi wananchi kuwapigia kura.

Kenya ni miongoni mwa mataifa ambayo raia wake wanakumbwa na hatari ya baa la njaa, uhaba wa maji, ukosefu wa ajira na mifumuko wa bei za bidhaa ambayo daima imesambaratisha maisha ya wengi. Hii ni kutokana na ongezeko la uhalifu, ugonjwa wa utapiamlo na vifo vya mifugo.

Hazi ni baadhi ya shida ambazo wakuu wa magatuzi wapya na watakaoshikilia hatamu ya pili watakumbana nazo. Shinikizo ni kubwa sana kutoka kwa wakenya ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi kwa ahadi za uongo huku waliowateua wakizidi kusowera.

Franklin Nakhitari ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Maseno ambaye alilazimika kukatiza masomo kutokana na ukosefu wa karo na hali ngumu ya maisha.Bidii yake ya kusaka msaada kutoka kwa wahisani hazikufua dafu.

“Ilinilazimu kukatiza masomo yangu hasa ambapo wazazi wangu hawangweza kulipa karo. Inasikitisha maanake nilikuwa mwaka wa tatu karibu kufanya mtihani wa mwisho wa muhula.Nilitembea kwa maofisi lakini sikufaulu,” Anasema Frank ambaye anasomea taaluma ya uanahabari.

Kwa upande wake Josephine Awour ambaye anasoma katika taasisi moja iliyoko kaunti ya Kisumu, anasema kwamba maisha yake yalibadilika baada ya kifo cha baba yake ambaye alikuwa akiugua ugonjwa wa saratani.

Josephine ambaye alizaliwa katika familia ya wana wanne, yeye na ndugu zake watatu, ilimlazimu kutafuta mbinu ya kujisaidia pamoja na familia yake maana mama yao mjane hana uwezo.

Alijitosa katika ukahaba licha ya umri wake[22]. Anasema hii inampa pesa za haraka na pia halipi kodi kubwa kama wafanyibiashara maduka.

“Sikuwa na la kufanya ila kujitosa kwenye hii biashara maana inanipa pesa za haraka angalau kununua chakula.Maisha yangu yalibadilika baada ya baba yangu kuaga dunia mwaka wa 2021,”Anasimulia Josephine.

Hali hii si tofauti na ile ya asilimia kubwa ya wakenya ambao wanagharamika kuwafundiha wanawe ambao baada ya kuhitimu vyuo vikuu au za kiufundi wanakumbana na jinamizi la ukosefu wa ajira na hali ngumu ya maisha.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na mdhibiti wa bajeti, Kaunti nyingi zina tatizo la madeni kulipa huduma za umeme, afya,na mishahara ya wafanyikazi miongoni mwa zingine.Hii itakuwa shida kwa Magavana kutekeleza miradi mipya au hata kukosa kufanikisha sehemu kubwa ya manifesto zao.

Wananchi wakati huu hawasikilia kisingio tena kama asemavyo Bw Charles Nyambuga ambaye ni mchanganuzi wa maswala ya siasa na uongozi.

Kulingana na yeye,viongozi walioteuliwa hasa baada ya kinya'nga'nyiro kikali, hawana budi kufanya kama walivyoahidi wapiga kura. Raia walisikia kila neno walilotamka, hakikisho lao la kubadilisha hali na kuboresha uchumi.

Sasa ni wakati wao kufanya kazi. Siasa na vioja vya kampeni vimepita.

View Comments