In Summary

• Wanjiru alidaiwa kujiua  baada ya kuamuriwa na mwalimu wake kunyoa nywele kama adhabu mnamo siku ya kuripoti shuleni kwa muhula wa tatu.

•Familia yake inasema kwamba alikuwa akijitenga na kusalia kimya lakini hawakutarajia kwa vyovyote vile angejitoa uhai.

Kitanzi
Image: HISANI

Familia moja eneo la Kaloleni , Kaunti ya Nakuru, inaomboleza kifo cha mtoto wao aliyejitia kitanzi baada ya kuagizwa na mwalimu wake kunyoa nywele.

Shamamcy Wanjiru mwenye umri wa miaka 16, alidaiwa kujiua  baada ya kuamuriwa na mwalimu wake kunyoa nywele kama adhabu mnamo siku ya kuripoti shuleni kwa muhula wa tatu.

"Alikuja nyumbani Jumatatu jioni akaambiwa na mwalimu wa darasa Jumanne asikuje shule akuje na mzazi sasa Jumatano kaenda akaambiwa anyone, alikuja nyumbani akiwa na hasira nikamwambia anyoe akasema atajua kama atanyoa," mmoja wa jamaa ya Wanjiru  aliambia kituo kimoja cha habari cha hapa nchini.

Kulingana na familia, Wanjiru alimwandikia mwalimu huyo barua ya kuomba msamaha, siku moja kabla ya kujitoa uhai.

Familia yake inasema kwamba alikuwa akijitenga na kusalia kimya lakini hawakutarajia kwa vyovyote vile angejitoa uhai.

Familia hiyo iliyoachwa na huzuni inasema kuwa mwanawe alikuwa na mustakabali mwema na masomo yake na aliazimia kuwa muuguzi.

"Alikuwa anasema kuwa anataka kuwa nurse. Sikudhani hiyo punishment alipewa ndio ingemcost maisha yake; walikuwa wasichama wawili. Huyo Mwalimu hakujua mtoto atatisha maisha yake juu ya kunyoa nywele," mmoja wa jamaa ya marehemu alielezea.

Hiki sio kisa cha kwanza cha mwanafunzi kujitoa uhai. Visa kama hivyo vimekuwa nikigonga vichwa vya habari mara kwa mara.

Mwezi  Septemba, kisa kingine kama hicho kiliripotiwa katika eneo la Matungulu, Kaunti ya Machakos ambako mwili wa mwanafunzi wa kidato cha tatu  ulipatikana ukining’inia chooni.

Mwanafunzi huyo alidaiwa kuiba shilingi 2,500 na penseli za mwanafunzi wenzake.

Kulingana na ujumbe wa kujitoa uhai alioacha, marehemu ulielezea kuwa watu walimshutumu kwa kuiba na kubainisha kuwa hakuna aliyemwamini hata aliposisitiza kuwa hana hatia.

Pia alimshukuru mama yake kwa usaidizi wake akisema kutatamisha maisha yake ilikuwa njia ya  kuhakikisha hamkatishi tamaa tena.

Mwanafunzi wa kidato mwenye umri wa miaka 17 alifariki katika kijiji cha Kona Mbaya eneo bunge la Likuyani kaunti ya Kakamega  baada ya kudaiwa kunywa sumu.

Iliripotiwa kuwa mwanafunzi huyu alikuwa akitishia kuacha shule akilalamika kuwa masomo yalikuwa magumu na ya kupoteza muda. Kijana huyo alijitoa uhai kwa kile alichodai kuwa kushinikizwa kuenda shule.

Vitendo hivi vimewaacha wazazi wakiwa na wasiwasi kuhusu maslahi ya wanao wao. Wengi  wakisema kuwa wamekuwa  na woga kuhusu hali ya watoto wao wakati wakiwa shuleni.

Ni jambo la  kuhuzunisha kuona wazazi wakiwatuma watoto wao shuleni wakiwa wazima na wenye afya na baadae taarifa ya kutoridhisha kutokea.

Sasa ni wito kwa serikali haswa waziri mpya  wa elimu Bwana Ezekiel Machogu kwa ushirikiano na jopo la walimu kutafuta suluhisho.

View Comments