In Summary

• Padri Francis alianza kwa kuweka wazi kwamba kanisa katoliki kwa njia yoyote halina uwezo wa kumzuia yeyote haki yake ya kuoa.

• Mtu kabla hajavikwa jukumu la upadri, hufanya uamuzi wake binafsi bila kushrutishwa, kujitenga mbali na suala la kufanya mapenzi au kuoa.

Mwanamke aliyekuwa anajifungua apoteza mtoto baada ya sista kukataa kutoa ambulensi kumkimbiza hospitalini.
Image: Maktaba// rozali

Wikendi iliyopita, habari za padri wa kanisa katoliki jimbo la Ruai zilienezwa kama moto wa jangwani baada ya kuripotiwa kufariki katika chumba cha wageni katika mgahawa mmoja kaunti ya Murang’a.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, padri huyo mwenye umri wa miaka 43 alikodisha chumba kwenye mgahawa huo siku ya Ijumaa akiwa na kidosho mmoja mwenye umri wa miaka 32.

Baadae Jumamosi aliripotiwa kuzirai na kukimbizwa hospitalini lakini akafa – jambo ambalo lilifunguliwa mirija ya habari mbalimbali kuhusu tukio hilo la kushangaza.

Wengi walibaki kujiuliza maswali mengi kuhusu mazingira mazima ya tukio lenyewe, ikizingatiwa kwamba ni kasisi wa kanisa katoliki ambao sheria yao kuu ni kwamba kuhani hafai kuoa wala kushiriki katika vitendo vya mapenzi, kwani kinadharia ni kama amekubali kutumikia kanisa.

Lakini je, ni mchakato gani unaofuatwa ikibainika kwamba kuhani wa kanisa katoliki ametuhumiwa kuvunja agano na kiapo cha kutojihusisha kimapenzi na mtu yeyote?

Ili kupata majibu haya, mwandishi wa tovuti hii aliwasiliana na hukani mmoja ambaye alitoa maelekezo jinsi suala hilo hushughulikiwa na kanisa katoliki ikiwa kasisi amepatikana na tuhuma za kufanya mapenzi au kuoa.

Katika Makala haya, tutamtambua padre huyo kwa jina lake moja tu – Francis.

Padri Francis alianza kwa kuweka wazi kwamba kanisa katoliki kwa njia yoyote halina uwezo wa kumzuia yeyote haki yake ya kuoa.

Mtu kabla hajavikwa jukumu la upadri, hufanya uamuzi wake binafsi bila kushrutishwa, kujitenga mbali na suala la kufanya mapenzi au kuoa.

“Kanisa halinyimi mtu yeyote fursa ya kuoa. Mtu Anachagua kwa mapenzi yake kutofunga ndoa akitegemea msaada kutoka kwa Mungu kuwa mwaminifu kwa nadhiri zake,” alisema padre Francis.

Padri Francis alisisitiza kwamba kwa mujibu wa kanuni za kanisa katoliki, mtu ukishavikwa taji la kuwa padri, hata ufanye makosa gani huwezi vuliwa taji hilo, bali utavuliwa tu mamlaka ya kufanya majukumu ya padri.

Francis alieleza kwamba taji la upadri ni kama kibali ambacho hutolewa na Mungu na hivyo ukishapewa hakuna kunyang’awa, ila hautaruhusiwa kuongoza ibada kama kasisi, miongoni mwa majukumu mengine.

“Anaendelea kuomba kwa ajili ya neema za Mungu ambazo hazikatishi tamaa. Au katika hali mbaya sana anaweza kuomba laicization (kuvuliwa mamlaka ya kuwa padri) kutoka Holy Sea. Kazi za upadri zinaondolewa kwake lakini anabaki kuwa padri. Hata hivyo, mara baada ya kuwekwa padri, mmoja ni padri milele kwa utaratibu wa Melkizedeki wa Kale,” alifafanua.

“Kazi za ukuhani hapa humaanisha kutoa sakramenti kwa mfano. Ubatizo, ndoa, kusikia maungamo,” aliongeza padri Francis.

Na je, iwapo padri amejipata katika tuhuma hizo, nani huitisha uchunguzi dhidi yake kutenganisha ukweli kutoka kwa uongo?

“Watu wa kawaida wa ndani (askofu) wanaweza kuuliza polisi kufanya hivyo,” alisema.

Padri Francis alisema mapadre wengi baada ya kuvuliwa mamlaka ya kuongoza kazi za kawaida za padre, huwa hawapotezi kitu kwani wengi wao huwa na biashara zao, nyumba na hata gari.

“Wengi wao wana magari, nyumba, biashara zao...padri anapata posho ndogo tu inayoitwa stipend,” Francis alisema.

Kwa upande wake, Padri mwingine maarufu nchini, Padri Kinyua alisema kwamba mapadre wa kanisa katoliki wanahitaji maombi hasa wakati huu, huku akisisitiza kwamba hata mapadri nao ni binadamu.

"Makuhani ni wanadamu wenye uwezo wa kuanguka katika dhambi. Ni kweli kwamba dhambi na makosa ya makuhani leo yameleta shida kwa waaminifu. Tumepitia kipindi ambacho makasisi wengi sana wamekuwa waasi, kutokuwa waaminifu kwa mafundisho ya Kanisa, wavivu, wasiojitayarisha kuhubiri, wasio na maombi, na wasio na heshima," Kinyua alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

View Comments