logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Watu wa jinsia mbili: ‘Nimefanyiwa upasuaji mara 39’

Denis Wamalwa ni Kamishna waTume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu nchini Kenya

image
na Davis Ojiambo

Habari26 October 2023 - 05:13

Muhtasari


  • • Watu wa jinsi mbili, ni watu wa kawaida ila madhila wanayopitia ni ya kuvunja moyo hata ingawa hali yao inahusisha maumbile ya Rabana.
  • • Daktari Denis Wamalwa, mtu wa kwanza wa jinsi mbili kushikilia ofisi ya serikali nchini Kenya.
ni Kamishna waTume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu nchini Kenya na ni mtu aliyezaliwa na jinsi mbili.

Hakuna kitu kinachokatisha tamaa kama mtu kuteseka kwa jambo ambalo liko nje ya uwezo wake. Nazungumzia jamii ambayo imekuwa nadra sana kuzungumziwa hasa kwa Afrika Mashariki.

Watu wa jinsi mbili, ni watu wa kawaida kama wale wengine ila madhila wanayopitia ni ya kuvunja moyo hata ingawa hali yao inahusisha maumbile ya Rabana.

Mwandishi wa BBC Asha Juma alizungumza na watu wawili waliozaliwa na jinsi mbili akiwemo Daktari Denis Wamalwa, mtu wa kwanza wa jinsi mbili kushikilia ofisi ya serikali nchini Kenya na mwathirika ambaye kwa leo tumempa jina la Samuel kwa sababu ya usalama wake ili kutathmini kile wanachopitia.

Daktari Denis Wamalwa ni Kamishna waTume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu nchini Kenya na ni mtu aliyezaliwa na jinsi mbili. Katika simulizi ya safari ya maisha yake, Wamalwa anabubujikwa na machozi anapoelezea kuhusu panda shuka zake maishani.

Safari ya maisha iliyojaa machungu

Punde tu nilipomuuliza alichopitia wakati wa ujana wake, Denis Wamalwa alishindwa kujizuia, alishusha pumzi kwa nguvu huku maneno yakisita kutoka kinywani mwake alipojiwa na kumbukumbu za aliokabiliana nayo.

‘’Ni safari ndefu, haijakuwa rahisi. Nimefanyiwa upasuaji mara 39 kwa zaidi ya saa mbili na saa kumi na mbili,’’ Wamalwa alisema.

‘’Watoto wa jinsi yangu wanaanza kubaguliwa baada tu ya kuzaliwa, nimejaa uchungu maisha yangu yote, sijakuwa na furaha. Upweke wa kuishi peke yako, singependa mtu yeyote apitie kile nimepitia na ndio tumeanza hii safari,’’ alisema Wamalwa.

Simulizi ya Wamalwa iliyojaa machungu haiko peke yake. Mtu ambaye nimempa jina ambalo sio lake, Samuel kwa usalama wake amelelewa kwa utambulisho wa mtoto wa kike lakini kadiri alivyoendelea kukua ndivyo mwili wake ulivyozidi kubadilika.

‘’Baba yangu alitoroka nilipozaliwa, sijawahi kumuona na sidhani kama nitawahi kumuona. Na mama yangu alishaaga dunia. Haikuwa rahisi,’’ Samuel alisema.

Ni wazi kuwa safari ya watoto wa jinsi mbili hasa katika ukuaji huwa na changamoto si haba.

Samuel anakumbuka wakati wake akisoma, alikuwa anafuatiliwa kwa karibu mno na mzazi wake.

Alipofikisha umri wa kubalahe, Samuel alikuwa akiona wenzake wanapewa sodo au pads kwa kiingereza akiwa amehifadhi elimu aliyopewa kuhusu wasichana wanapovunja ungo lakini cha kushangaza, hakuwahi kupata hedhi.

Anachokumbuka Samuel ni kwamba hadi sasa, ‘’wale wadogo zangu wananiita kaka yao lakini wale wakubwa zangu wananiita dada yao kwasababu tulikuwa pamoja kipindi mama alivyonilea namna alivyotaka yeye.’’

Na isitoshe, maisha ya shule ya Samuel yalikuwa magumu kwani licha ya kwamba alikuwa amevishwa sketi na mama yake, yeye alishiriki michezo ya kiume na pia alipenda kwenda choo cha wavulana.

Na mwisho wa siku akaishia kubadilishwa shule moja hadi nyingine akiwa na matumaini kuna ile ingemkubali kama mwanamume. Hata hivyo, iliishia kuwa ndoto ambayo haikuwahi kutimia.

‘’Cheti changu cha kuzaliwa kilikuwa kimenitambulisha kama msichana, kwa hiyo hakuna aliyetaka nijiunge na shule ya wavulana ,’’ Samuel anasema.

Maswali magumu yasio na majibu

Kitu cha msingi ambacho ni muhimu kufahamu ni kwamba watu wa jinsi mbili sio jambo ambalo mtu anachagua ila ni namna anavyozaliwa.

Lakini pengine kwa sababu ya ukosefu wa uelewa, jamii mara nyingi huwa inajaribu kila mbinu kutafuta njia ya kubadilisha hali hii licha ya ukweli kwamba ni maumbile ya mtu. Samuel anazungumzia changamoto kubwa ambayo amepitia maishani mwake.

‘’Changamoto kubwa ambayo nimepitia ni jamii, utamaduni wetu, mtu pekee ambaye anakuelewa ni mzazi wako, lakini mzazi akishaondoka, ni kama jamii nzima haikutambui.’’

‘’Nimepelekwa kwa maombi, kwa waganga hakuna pahali sijapelekwa, hadi wengine wanakuambia ni ruhani mke ndio anakufanya unakuwa hivyo, wengine wanasema ni mapepo. Nimepitia mambo mengi sana,’’ Samuel anaongeza.

Kwanini Samuel anafikiria hili ni suala ambalo linafaa kuzungumziwa kwa uwazi.

‘’Kwa sababu, ushawahi kujiuliza mtu wa jinsi mbili anavaa padi inakaa vipi? Je kwa wenye wanaenda kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi watahudumiwa vipi hasa ukizingatia kuwa maumbile yetu ni tofauti? Ni mipira gani ya kondomu inaweza kunitosha?

Ni baadhi tu ya maswali ambayo Samuel anaona kufikia sasa, yamekosa majibu.

Watu wa jinsi mbili wako vipi kimaumbile

Wakati mtoto anazaliwa, kawaida iwapo itakuwa ni hospitali, mama hufahamishwa na hata kuonyeshwa kwa macho ama amejifungua mtoto wa kiume au wa kike.

Lakini kuna uwezekano mkubwa wa kutokea mchanganyiko iwapo mtoto atakayezaliwa atakuwa ni wa jinsi mbili.

kwa sababu kwa macho ya kawaida, kinachoonekana huwa hakiko wazi moja kwa moja kama ilivyozoeleka.

Na mabadiliko kamili huendelea kujitokeza kadiri mtoto anavyoendelea kukua hasa akitimiza muda wa kubalehe.

Hata hivyo, mabadliko makubwa mno huwa ndani ya mwili, yaani kitu kisichoweza kuonekana kwa macho ya kawaida, moja kwa moja.

Kulingana na kamishna wa Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu nchini Kenya Dkt. Denis Wamalwa, ‘’wengi huwa wana tumbo la uzazi na korodani kwa pamoja,’’ huku akiendelea kueleza hali yake jinsi alivyo na kromosomu X ya ziada.

‘’Mimi niko na 46 X X Y kromosomu, ikimaanisha kuwa nimeegemea sana kwa mwanamke,’’ Wamalwa anasema.

Pengine hali kama hii ndio hufanya mtoto kubadilika kimaumbile, utaona alilelewa kama msichana, ikifika wakati wa kubalehe, anabadilika na kuwa mvulana au kinyume chake kulingana na mabadiliko yake kimwili yalivyo.

Matumaini ya siku za baadaye

Kwa jicho la kawaida unaweza kusema watu wa jinsi mbili ni suala ambalo limefumbiwa jicho kwa karne nyingi kote duniani lakini hatimaye mwanga wa matumaini unang’aa.

Katika nchi za Afrika, Kenya imepiga hatua ikiwa tayari imetayarisha mswaada kwa jina Intersex Bill 2023, ambao unasubiriwa kujadiliwa bungeni kabla ya kuwa sheria.

Huku maadhimisho ya watu wa jinsi mbili yakifanyika tarehe 26 mwezi wa 10 kila, Denis Wamalwa kutoka shirika la Kutetea Haki za Binadamu Kenya, amekuwa miongoni mwa jopo lenye kuhusika katika maandalizi ya mswada huo na anasema baadhi ya malengo muhimu ni watu wa jinsi mbili watambuliwe na sheria na serikali na wapewe matibabu stahiki kama wengine.

‘’Mswada huu unapendekeza wapewe ajira jinsi walivyo bila kubaguliwa, na pia unaangazia iwapo mtu wa aina hii atajipata katika mkono mbaya wa sheria atafungwa wapi? Kuna hofu kwamba watu wa jinsi mbili wakijipata katika hali hii, watakuwa katika hatari ya kunyanyaswa,’’ Wamalwa amesema.

Kuzaliwa kama mtu wa jinsi mbili, sio dhambi, laana wala makosa. Ni maumbile tu. Hata ingawa pengine bado kuna nchi nyingi ambazo zinaonekana kuwa katika giza kuhusu suala hili, juhudi zinazofanywa nchini Kenya na kwingineko, huenda zikawa chachu ya mabadiliko na mwamko mpya wa kuboresha maisha ya watu wa jinsi mbili, ili kuwawezesha kuwa na fursa sawa ya kuchangia kikamilifu katika masuala ya jamii.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved