In Summary

•Diana Sermetei, 17, amesema kuwa alikuwa amempeleka binti yake Phoebe Surumbati  kliniki siku ya Jumanne wakati mwanamke mmoja alikuja kwake na kujitambulisha kama mfanyikazi wa hospitali hiyo.

•Diana alisema kwamba mwanamke aliyechukua bintiye alimwambia kuwa hospitali ile huzawadi kina mama wote baada ya kuhudumiwa na akajitolea kumsaidia kushika mtoto wakat yeye anapanga foleni ili kupokea zawadi.

Mtoto wa mwezi mmoja aliyeibiwa
Image: ROP JANET

HABARI NA ROP JANET

Mwanamke mmoja kutoka kijiji cha Esokota kaunti ya Kaijado anamtafuta mtoto wake wa wiki sita ambaye aliibiwa na mwanamke aliyejifanya kuwa muuguzi katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kajiado.

Diana Sermetei, 17, amesema kuwa alikuwa amempeleka binti yake Phoebe Surumbati  kliniki siku ya Jumanne wakati mwanamke mmoja alikuja kwake na kujitambulisha kama mfanyikazi wa hospitali hiyo.

'Muuguzi' huyo bandia alimwambia Diana kuwa angempa zawadi kwa kumpeleka bintiye kupata chanjo baada ya kufikisha wiki sita na kusema kuwa hiyo ni  desturi ya hospitali hiyo.

Diana alisema kwamba mwanamke aliyechukua bintiye alimwambia kuwa hospitali ile huzawadi kina mama wote baada ya kuhudumiwa na akajitolea kumsaidia kushika mtoto wakat yeye anapanga foleni ili kupokea zawadi.

Baada ya Diana kusimama kwa foleni kwa kipindi cha dakika chache aligeuka na kumkosa mwanamke aliyeachia mtoto amsaidie kushika.

Hapo akaanza kupiga nduru ila mwizi yule alikuwa ashatoweka na binti yake.

Picha za CCTV zilionyesha mwanamke mmoja akiingia hospitalini akiwa pekee yake mida ya saa mbili asubuhi na kuondoka akiwa na mtoto mida ya saa saba alasiri.

Mwanamke huyo alionekana akiwa anasemamisha bodaboda na kubebwa kuelekea upande wa mji wa Kajiado.

Diana ametoa ombi kwa yeyote ambaye ana habari zozote kuhusu tukio hilo kumsaidia kupata bintiye ambaye amekuwa naye kwa kipindi cha wiki sita tu.

View Comments