In Summary
  • Kulingana na Raila, Wakenya lazima waishi kwa raha na wasilazimike kulala njaa wakati wowote
Image: TWITTER// RAILA ODINGA

Kiongozi wa ODM Raila Odinga amesema kuwa msukumo wake wa kutafuta urais ni kusukuma maisha bora kwa kila Mkenya.

Kulingana na Raila, Wakenya lazima waishi kwa raha na wasilazimike kulala njaa wakati wowote.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema ana imani kwamba hilo linawezekana na kwamba siku bora zaidi zinakuja.

"Tunasukuma maisha bora kwa kila Mkenya kote nchini. Ni lazima watu wetu waishi maisha ya starehe na wasilazimike kulala njaa, tutafanya hili! Siku bora zinakuja," Raila alisema.

Raila atakuwa akisaka wadhifa wa juu nchini kwa mara ya tano. Wakati huu, anatazamiwa kuchuana vikali na Naibu Rais William Ruto wa Muungano wa Kenya Kwanza.

Raila kama vile mshindani wake amekuwa akizunguka nchi nzima akifanya kampeni huku akiuza ajenda yake kwa watu.

Hata hivyo, amepumzika kwa wiki moja kwenye kampeni huku chama chake kikiendesha kura za mchujo.

ODM itakuwa ikifanya uteuzi wake wa mwisho jijini Nairobi mnamo Aprili 21.

Waziri Mkuu huyo wa zamani pia anatarajiwa kuondoka nchini Aprili 21, kwa safari ya Marekani.

Raila atakuwa na shughuli nyingi nchini Marekani, akikutana na maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Marekani, jumuiya ya wafanyabiashara, viongozi wa kidini na Wakenya wanaoishi Amerika.

Msemaji wa sekretarieti ya kampeni ya Raila Makau Mutua alithibitisha safari hiyo lakini hakutoa maelezo zaidi.

Alisema watatoa mawasiliano kuhusu ziara ya Marekani kwa wakati ufaao.

 

 

 

View Comments