In Summary

•Msemaji wa polisi Bruno Shioso alisema matamshi ya Malala yanadhalilisha sana na yanalenga kukashifu taaluma ambayo imetukuka.

•Shioso aliweka wazi kuwa maarifa ni hitaji kubwa katika huduma ya polisi na bunduki ni chombo cha ziada tu cha kuwezesha kazi zao.

Seneta Cleopas Malala akihutubia wakazi wa Kakamega
Image: HILTON OTENYO

Kitengo cha polisi kimeeleza kusikitishwa kwao na matamshi ya seneta wa Kakamega Cleopas Malala kuwa elimu sio mojawapo ya sifa zinazohitajika ili kujiunga na huduma hiyo.

Kupitia taarifa iliyotolewa Jumatano jioni, msemaji wa polisi Bruno Shioso alisema matamshi ya Malala yanadhalilisha sana na yanalenga kukashifu taaluma ambayo imetukuka.

Shioso alisema matamshi ambayo seneta huyo alitoa Jumanne katika mkutano wa Kenya Kwanza mjini Kakamega hayafai na ni yanaudhi.

"Tumesikitishwa zaidi kwa kuwa matamshi haya ya kusikitisha yalitolewa na kiongozi ambaye sio tu kwamba tunamheshimu sana lakini pia tunaendelea kumpatia ulinzi wa siku nzima  kwa fahari na umahiri," Shioso alisema.

Aliweka wazi kuwa maarifa ni hitaji kubwa katika huduma ya polisi na bunduki ni chombo cha ziada tu cha kuwezesha kazi zao.

Msemaji huyo wa polisi pia alieleza kuwa elimu ni kiungo muhimu sana katika taaluma hiyo kwa kuwa inawawezesha maafisa kuelewa mafunzo zaidi wanayopatiwa ili kupanua uwezo wao.

"NPS inachukua fursa hii kuwahakikishia maafisa wote wakiwemo Wakenya nia njema kupuuza maoni hayo hasi yaliyotolewa na Seneta, ambayo yanalenga tu kusababisha kutoridhika miongoni mwa maafisa wa kitengo cha usalama, na hivyo yachukueni kwa dharau kabisa yanayostahili," Alisema Shioso.

Aidha alitoa hakikisho kuwa Inspekta Generali wa Polisi Hillary Mutyambai ataendelea kuboresha huduma hiyo na kusaidia kulinda usalama wa nchi.

Siku ya Jumatano, video ya Malala akisema maafisa wa polisi hawahitaji elimu kutekeleza majukumu yao ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua hisia tofauti.

Seneta huyo anayewania kiti cha Ugavana wa Kakamega, alisema kazi ya polisi inahusisha tu uwezo wa kushika bunduki.

"Si kazi ya polisi nikushika tuu bunduki?" Malala alisema.

Alisema waliofaulu mitihani waruhusiwe kuendelea na masomo katika vyuo vikuu na kuongeza waliokatisha masomo waajiriwe katika kitengo cha polisi.

View Comments