In Summary

• “Willie, licha ya kutoka familia ya kimaskini, alikuwa mtu mpole na mkarimu sana, ni mtu alikuwa amejiweka vizuri" - Hannah Wanjiku ambaye ni mjane wa wakili Kimani.

Hanna Wanjiku, mjane wa wakili Willie Kimani akiwa katika hali ya kusononeka.
Image: Screengrab//AfricaUncensored YouTube

Hanna Wanjiku, ambaye ni mkewe wakili Willie Kimani aliyeuawa mwaka wa 2016 pamoja na mteja wake na dereva wa teksi katika njia za kutatanisha baada ya kudaiwa kutekwa nyara na polisi amekumbuka kwa uchungu jinsi ambavyo mapenzi yake na wakili huyo marehemu yalivyochipukia.

Akizungumza na mwanahabari wa ufichuzi John Allan Namu katika Makala ambayo mwanahabari huyo ameachia jana kwa mada ‘Justice Be Our Shield’ Wanjiku alishindwa kujizuia akielezea kumbukumbu za huba lao ambalo lilikatizwa ghafla mikononi mwa polisi katili, kosa la Kimani likiwa kuwakilisha mteja wake mahakamani.

Wanjiku alisema kwamba mapenzi yao yaliota pindi tu Kimani alipohitimu kutoka chuo kikuu na digrii ya sheria. Wanjiku alikuwa anatoka katika familia yenye kipato cha kadri ilhali Kimani alikuwa anatoka familia ya uhayawinde mkubwa, lakini utabaka huu haukukatisha mahaba yao kwani walikuwa wamekula Yamini kuishi pamoja kama mke na mme.

“Willie, licha ya kutoka familia ya kimaskini, alikuwa mtu mpole na mkarimu sana, ni mtu alikuwa amejiweka vizuri na ni mtu ambaye alikuwa anazungumza kitu alichokuwa akikitaka kwake mwenyewe na pia kwa familia yake, Alikuwa na ndoto moja aliyokuwa ameiandika kwenye daftari lake, ambayo nilikuja kuiona baadaye sana baada ya kufariki..,” Wanjiku alieleza baina ya kwikwi za kumbukumbu hizo za kutia huruma, huku akishindwa kumaliza kuongea.

Kesi dhidi ya polisi walioshukiwa kushiriki mauaji ya wakili huyo, mteja wake pamoja na dereva wa teksi aliyewabeba kutoka mahakama ya Mavoko mnamo mwezi Juni mwaka 2016 imekuwa ikiendelea kwa miaka sita sasa ambapo wiki moja iliyopita maafisa hao walipatikana na hatia ya mauaji ya watatu hao.

Maafisa hao wa polisi waliotumika kutekeleza ukatili huu ni pamoja na Fredrick Leliman, Stephen Cheburet, Sylvia Wanjiku, na mpelelezi wa polisi Peter Ngugi ambao wote walisemekana kushiriki kwa njia moja au nyingine katika maovu hayo ambayo yaliacha kovu la kudumu katika familia za Kimani, mteja wake na dereva mhudumu wa teksi

View Comments