In Summary

• Maafisa hao wameagizwa kukabidhi afisi zao kwa wakurugenzi wa idara huku gavana akianzisha harakati za kulainisha huduma za kaunti.

Gavana wa Busia Paul Otuoma (katikati) akiwa na Naibu wake Athur Odera (kushoto) akitangaza kuwatuma kwa likizo ya lazima mawaziri wa kaunti. PICHA/Paul Otuoma FACEBOOK.

Gavana wa Busia Paul Otuoma amewatuma kwa likizo ya lazima mawaziri wote, maafisa wakuu na Katibu wa kaunti, Nicodemus Mulaku kwa likizo ya lazima. Agizo hilo, Otuoma alisema siku ya Alhamisi linaanza kutekelezwa mara moja. 

Maafisa hao wameagizwa kukabidhi afisi zao kwa wakurugenzi wa idara huku gavana akianzisha harakati za kulainisha huduma za kaunti.

 Otuoma amekuwa mara kwa mara, tangu wakati wa kampeni akisema kuwa miongoni mwa kazi za kwanza atakazofanya kama gavana ni kunadhifisha  serikali ya kaunti na kuhakikisha utoaji wa huduma unaboreka.

 "Ninataka kutangaza hapa leo (Alhamisi) kwamba ninamtuma Katibu wa kaunti ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya mpito kwa likizo ya lazima," Otuoma alisema kwenye kikao na wanahabari katika uwanja wa Busia ATC. 

"Mawaziri wote (CEC) na maafisa wakuu wote (CO) pia wanatumwa kwa likizo ya lazima mara moja." 

Gavana huyo ambaye alikuwa ameandamana na naibu wake Arthur Odera, Mwenyekiti wa Bodi ya Utumishi wa Umma katika Kaunti Assumpta Obore na Mkurugenzi wa Utawala na Mipango Maalum Timothy Odende alifichua kwamba jopokazi la RRI litajumuisha naibu wake Arthur Odera ambaye atakuwa mwenyekiti wa kamati ndogo ya Fedha, Uchumi, Mipango na ICT.

Pia katika jopo kazi hilo, kutakuwa na Mbunge wa zamani wa Butula, Michael Onyura ambaye atakuwa mwenyekiti wa kamati ndogo ya Usimamizi, Utawala, Sheria na Utumishi wa Umma huku Dkt Olango Onudi akiwa mwenyekiti wa kamati ndogo ya Afya, Elimu, Miundombinu na Jamii. Patrick Sanya Odame atakuwa mwenyekiti wa kamati ndogo ya Kilimo, Maji, Biashara na Ardhi huku Odende akiwa Katibu wa jopo hilo. 

Gavana alisema majina ya wajumbe wengine wa kamati ya kikosi kazi hicho yatawasilishwa baadaye. 

"Pia nimeagiza kwamba majukumu ya Manispaa ya Busia ambayo yalikuwa yakimilikiwa na idara ya Ardhi Nyumba na ustawi wa Miji yahamishwe kwa bodi mara moja ili kutekelezwa ipasavyo kama ilivyoainishwa katika sheria," Otuoma alisema. 

Alisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha utawala wake unatimiza wajibu wake kama alivyoahidi wakati wa kampeni. 

"Tunatarajia kamati hizi kutekeleza majukumu ambayo tumeweka mbele ndani ya siku 100 za RRI na tutakuwa na utathmini baada ya kila siku 25," Otuoma aliongeza.

Gavana huyo alitoa tangazo hilo siku mbili baada ya kuwaambia wafanyikazi wa kaunti kutanguliza utoaji huduma bora kwa wakaazi wa kaunti hiyo huku akianza kuunda utawala ambao utasimamia shughuli kwa miaka mitano ijayo. 

Mnamo Jumanne baada ya mkutano alioitisha mjini Busia na kuhudhuriwa na mawaziri, maafisa wakuu na wakurugenzi wa idara, Otuoma alisema wafanyikazi wavivu hawatakuwa na nafasi katika serikali yake. 

"Watumishi wa umma lazima waelekezwe ili wajue kuwa serikali ya wakati huu haikubali tabia fulani," Otuoma alisema. 

“Kwa wale ambao wamekuwa wakifanya mambo kwa namna fulani, wanafaa sasa kujua kwamba lazima pawepo na mabadiliko katika fikra zetu katika namna ya kufanya mambo ili kuiana na serikali mpya la sivyo hatua zichukuliwe dhidi yao.” 

Gavana Otuoma alitilia mkazo sana utoaji wa huduma, matumizi bora ya rasilimali za kaunti na kutafuta njia mpya za kuzalisha pato zaidi kwa kaunti ili kupiga jeki utoaji wa huduma kwa wananachi.

View Comments