In Summary

• Alisema iwapo hupendi kelele basi subiri gari ambali halina sauti.

• Sakaja pia  alisema anaunga mkono wahudumu wa matatu walioweka grafiti kwenye magari yao.

Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja
Image: Facebook

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja amepuuzilia mbali malalamishi yaliotolewa kwake kuwazima wahudumu wa magari ya umma wanaoweka sauti ya juu ya muziki kwenye magari yao.

Sakaja alisema anaunga mkono wahudumu wa matatu ambao pia walioweka grafiti kwenye magari yao akisema huo ni urembo na ni utamaduni wa Nairobi.

"Eti mambo ati graffiti na muziki kwa matatu ati ni mbaya, hio ni ufala. Huu ni utamaduni wetu."  alisema Sakaja.

Gavana alisema madereva wana uhuru wa kuchora magari yao na kujiamulia kinachowafaa wasafiri.

"Kama mtu anataka matatu haina muziki angojee aingie yenye haina muziki na kama mtu anataka kusema iko na ngoma aingie yenye iko na ngoma," Sakaja alisema.

Zaidi ya hayo Sakaja aliongeza kuwa atakuwa anawapiga jeki na kuwapa tuzo wahudumu wa matatu pamoja na Saccos zinazofanya vizuri kwa kuzingatia nidhamu.

Katika utawala wa aliyekuwa rais mustaafu Uhuru Kenyatta alikuwa ameiamuru halmashauri ya NTSA kuruhusu michoro  kwenye matatu zao. 

NTSA hata hivyo  ilionya dhidi ya matumizi ya michoro inayouudhi na kuchukiza au maneno yanayochukiza pamoja na picha au ishara.

View Comments