In Summary

•Wakaazi wanadai ndovu hao ni wale waliotoroka kutoka mbuga ya wanyama ya Tsavo na sasa wanataka KWS kuchukua hatua za kuwakabili.

Ndovu wamuua mtu Kwale
Image: BBC NEWS

Mtu mmoja amuawa baada ya kushambuliwa na ndovu katika kijiji cha Mnarani kaunti ya Kwale huku makumi ya ndovu wakiendelea kuwahangaisha wakazi wa eneo la Shimba Hills na Lungalunga kwenye kaunti hiyo ya Pwani ya Kenya.

Kulingana na taarifa iliyopeperushwa na kituo cha runinga cha Citizen, mwathiriwa alikumbana na mauti usiku alipokuwa akielekea nyumbani kwake alipovamiwa na ndovu wanaorandaranda maeneo hayo baada ya kudaiwa kutoroka kutoka mbuga ya kitaifa ya wanyamapori ya Tsavo.

Katika eneo la Shimba Hills, wakazi pia wanakadiria hasara kubwa baada ya ndovu hao wengi kuvamia mashamba yao na kuharibu chakula.Wakazi hao sasa wanatoa wito kwa maafisa wa idara ya wanyamapori KWS kuwahi kwa haraka ili kuwaondoa wanyama hao hatari kabla ya kusababisha hasara zaidi na pia kusababisha maafa.

Kina mama katika kaunti hiyo walisema sasa wameingiwa na woga wa kukumbana na ndovu njiani wakitembea kilomita kadhaa kwa ajili ya kutafuta maji, ambapo pia wanyama hao nao wanajitokeza kwa wiki kukata kiu katika mito hiyo.

Wakaazi walisema kuwa ndovu hao hawasazi kitu chochote shambani kwani wanakula mahindi, minazi, migomba, huku pia wakisema ndovu huyo ni mkubwa asiyeweza kuzuilika.

Kando na kero la ndovu, wakaazi hao pia walisema nyani na tumbili ni wanyama wengine ambao wamekuwa wakiwahangaisha katika mashamba yao, huku wakiharibu vyakula vingi na kuacha jamii hiyo ikijikuna kwa njaa.

 

View Comments