Aliyekuwa mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando ametangaza kuondoka rasmi katika chama cha Narc Kenya huku akitaka msajili wa vyama vya kisiasa kumuondoa mara moja katika orodha ya wanachama wa chama hicho kinachoongozwa na Martha Karua.
Kabando alisema kuwa ni muda sasa aaanze kutafakari safari yake ya kisiasa akiwa na watu wenye mawazo kama yeye.
Alimtakia Karua na chama hicho kila la heri katika mikakati yao ndani ya muungano wa Azimio huku akidokeza kwamba yeye anaamini sana katika uongozi, ushirikiano na kufanya kazi kwa haki na kweli.
“Kama suala la dhamiri na kanuni, nimeagiza @ORPPKenya kufuta usajili wangu, mimi Mhe. Kabando wa Kabando, kutoka @narckenya. Ninaamini katika kazi ya pamoja ya uongozi na uaminifu. Nachukia ufisadi na ufisadi. Nashukuru @MarthaKarua na kumtakia heri katika shughuli za Azimio,” Kabando alisema.
Kabando alidokeza kushirikiana na uongozi wa rais Ruto kuanzia sasa kwenda mbele.
“Nitaendelea kwa ujasiri na kwa kujitegemea, au kwa kushirikiana na watu wenye nia sawa, nitatekeleza sehemu yangu ya kizalendo ili kudhibiti utawala mbovu wa Rais Ruto. Cha kusikitisha ni kwamba, si ODM wala NarcK wanaofanya kazi kitaasisi katika jitihada hii. Siasa za kitamaduni ni mbaya kwa demokrasia.”
Kabando alikuwa anawania useneta katika kaunti ya Nyeri akitumia chama cha Narc ambacho kilikuwa kimoja katika muungano pana wa Azimio la Umoja uliokuwa ukiongozwa na Raila na Martha Karua kama mgombea mwenza.