In Summary
  • Akiwa kwenye mahojiano Natembeya alisema kwamba aligundua hili alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Bonde la Ufa (RC) kwa miaka mitatu
gavana george natembeya
Image: hisani

Raia wa Nairobi wanafadhili majambazi katika eneo la North-Rift kwa kula nyama kutoka kwa ng'ombe walioibiwa na wezi hao, haya ni matamshi ya gavana wa Trans-Nzoia George Natembeya.

Kulingana na Gavana Natembeya, wanyama walioibiwa na majambazi husafirishwa hadi kwenye vichinjio vya Nairobi, kama vile vilivyoko Dagoretti, na hatimaye kuwa vyanzo vya masoko ya humu nchini.

Akiwa kwenye mahojiano Natembeya alisema kwamba aligundua hili alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Bonde la Ufa (RC) kwa miaka mitatu.

Aliendelea kusema kuwa kuna "cartel" nyuma ya usafirishaji wa mifugo, na kwamba askari polisi wote walio katika vizuizi mbalimbali barabarani wameingiliwa na rushwa.

"Wanyama hawa wanaliwa na watu wema wa Nairobi, nyinyi mnafadhili majambazi katika Bonde la Ufa na hii ni kauli ya ukweli sidhanii kwa sababu wanyama 1,000 wakiibiwa na kupelekwa katika Hifadhi ya Mazingira ya Laikipia kwa mfano lakini wanatoweka," alisema.

"Hata tulitoa maagizo kwamba wanyama wasisafirishwe baada ya saa kumi na mbili jioni na tuliwaagiza maafisa wetu wa polisi kuweka vizuizi vyote vya barabarani kutoka Baringo hadi Nairobi lakini vikundi hivi vinafahamu ni nani aliye kwenye kizuizi hicho. Wanabeba pesa na kuafikiana kila mtu," akaongeza.

"Ukijaribu kwenda kwenye machinjio ya Dagoretti ukajaribu kutafuta pembe za wanyama waliochinjwa huko hutapata maana watu wanawatambulisha ng'ombe wao na pembe zao. Hutapata chochote ikiwemo ngozi."

Natembeya aliongeza kuwa wakati akihudumu kama RC, juhudi za kukabiliana na tishio hilo  zilivunjika licha ya bidii yake kwa sababu hakukuwa na msaada wowote kutoka kwa serikali na maafisa waliotumwa mkoani humo waliachwa.

"Nilipoenda Bonde la Ufa nilisema nitakuwa Kamishna wa mwisho  kuzungumzia ujambazi. Nilikuwa na shauku kubwa na nilikusanya vyombo vyote vya usalama kutoka Turkana hadi Baragoi nilifanya mikutano na makamanda wote na aliwaambia kwamba ‘tuteseke kwa muda wa miezi miwili au mitatu lakini mtu mwingine yeyote anayekuja baada yetu asiteseke jinsi mlivyoteseka’,” alibainisha.

"Tulichoomba kutoka kwa serikali ni msaada wa angani na mafuta ya kutosha kwa magari yetu na idhini ya kuingia. Tuligawanya North-Rift katika sekta na makamanda wangu walikuwa tayari, wakasema wafe lakini wafe wakiwalinda Wakenya. Hatukupewa idhini hiyo,' alibainisha.

Gavana Natembeya alisema kuwa haziwezi kuwa na ufanisi kwa sababu wanajeshi hao wamekata tamaa, akibainisha kuwa hata upatikanaji wa mahitaji muhimu hauwezekani.

 

 

 

 

 

 

View Comments