In Summary

• Rais pia alitangaza kuwa serikali itaweka bilioni 20 kuhakikisha maafisa wanapata silaha za kukabiliana na wezi wa mifugo.

Rais William Ruto akitoa marufuku kwa wafugaji kutumia bunduki.
Image: Facebook

Rais William Ruto ametangaza marufuku ya wafugaji wote kulinda mifugo wao kwa kutumia silaha kali kama bunduki.

Hii imetajwa kama njia moja ya kujaribu kudhibiti mauaji na mashambulizi yanayoendelea katika maeneo ya ufugaji kakazini mwa Bonde la Ufa.

Rais alitangaza marufuku hii wikendi iliyopita katika kaunti ya Lamu ambapo alisema wafugaji wote sasa wanafaa kutumia fimbo kulinda mifugo.

Yeyote atakayepatikana akichunga mifgo kwa kutumia bunduki atachukuliwa hatua za kisheria kama jambazi.

Ruto alisema kuwa serikali yake imejitolea kukabiliana na tatizo la wizi wa mifugo haswa katika eneo la North Rift huku akifichua kwamba tayari wametenga bilioni 20 kushughulikia tatizo hilo.

“Hakuna mtu ataruhusiwa kutembea na bunduki eti anachunga ng’ombe. Kila mtu atafute fimbo achunge nayo ng’ombe. Mambo ya bunduki achia askari. Nimetangaza juzi kwamba tunaweka bilioni 20 kwa askari wetu kuwa na silaha za kutosha kuweka usalama katika taifa letu,” rais Ruto alisema.

Maeneo mengi ya ufugaji kama Suguta Valley, Kainuk, Tiaty, Kapedo na maeneo mengine ni kawaida kwa wafugaji kutembea na mifugo wao wakiwa wamebeba bunduki zao mabegani mwao kama njia moja ya kuweka usalama kutoka kwa wezi wa mifugo.

Jamii za Pokot na Turkana zimekuwa zikihasimiana kwa muda mrefu, huku mifugo wakiibwa kutoka jamii moja kwenda jamii nyingine, jambo ambalo limeathiri usalama kwa kukumbwa na vita vya kila muda.

View Comments